Kisumu: Polisi 6, raia 6 wapatikana wakipiga maji baada ya masaa ya amri ya kutotoka nje

Wote walipelekwa katika kituo cha polisi cha Kondele baada ya kukamatwa.

Muhtasari

•Kumi na wawili hao walipatikana wakiwa walevi katika baa ya Black Pearl pande ya Nyamasaria mida ya saa mbili usiku ambayo ni baada ya masaa ya amri ya kutotoka nje iliyopeanwa maeneo hayo.

Pingu
Image: Radio Jambo

Watu kumi na wawili ikiwemo polisi 6 miongoni mwao walijipata upande mbaya wa sheria usiku wa Jumamosi  baada ya kupatikana wakiwa wanakiuka mikakati iliyowekwa kudhibiti virusi vya Korona katika kaunti ya Kisumu.

Kumi na wawili hao walipatikana wakiwa walevi katika baa ya Black Pearl pande ya Nyamasaria mida ya saa mbili usiku ambayo ni baada ya masaa ya amri ya kutotoka nje iliyopeanwa maeneo hayo.

Ripoti ya polisi iliashiria kuwa tano kati yao; Daniel Maina,  Stanley Kimato, Angima Harret, Reuben Ngelech na Vine Okenyo walikuwa wametoka katika kituo cha polisi cha Nyagacho kaunti ya Kericho huku mmoja kwa jina John Ongweno akiwa ametoka  kituo cha Central kaunti ya Nakuru.

Raia waliopatikana ni pamoja na Juliet Cheruto, Eldqueen Wanjala, Mary Achieng, Maureen Adhiambo, Ronald Orengo na Peter Njuguna.

Wote walipelekwa katika kituo cha polisi cha Kondele baada ya kukamatwa.

Haya yanajiri baada ya serikali kubadilisha amri ya kutotoka nje katika kaunti 13 za eneo la magharibi mwa Kenya kutoka saa nne usiku kuja saa moja usiku baada ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya Korona..

Kaunti zilizoathirika ni pamoja na Kisumu, Migori, Trans Nzoia, Kericho, Bomet, Bungoma, Busia, Vihiga,  Homa Bay, Kisii, Nyamira, Siaya na Kakamega.