DCI wasihi wahasiriwa wa wizi jijini Nairobi kupiga ripoti rasmi

Hii ni baada ya maafisa hao kugundua kuwa Wakenya wengi wamekuwa wakieleza masaibu yao kwenye mitandao ya kijamii.

Muhtasari

•Wameeleza kuwa mara nyingi washukiwa wa wizi kwenye mitaa ya Nairobi huachiliwa huru baada ya kukamatwa kwani wahasiriwa wachache ambao hupiga ripoti katika vituo vya polisi huwa hawafiki mahakamani kuhudhuria kesi hizo.

•Siku ya Jumatatu, Wakenya wenye ghadhabu walishambulia kikundi cha watu walioshukiwa kuwa watapeli katika eneo la Archives na kuharibu mali na gari lao.

Mkuu wa idara ya DCI George Kinoti
Mkuu wa idara ya DCI George Kinoti

Maafisa wa DCI wameshauri Wakenya ambao wamejipata au watakaojipata mikononi mwa wakora wa kuny'ang'anya katika jiji la Nairobi kupiga ripoti rasmi katika ofisi za DCI za Nairobi ya kati.

Hii ni baada ya maafisa hao kugundua kuwa Wakenya wengi wamekuwa wakieleza masaibu yao kwenye mitandao ya kijamii.

"Wakati wahasiriwa wengi wanatumia mitandao ya kijamii kusimulia yaliyowapata mikononi mwa wezi (ambacho ni kitendo kizuri cha uhamasishaji), tunawasihi kufanya malalamishi hayo kuwa rasmi ili kuwezesha kuendeleza mashtaka wakati wezi wale wanakamatwa" maafisa wa DCI walisema kupitia mtandao wa Twitter.

Wameeleza kuwa mara nyingi washukiwa wa wizi kwenye mitaa ya Nairobi huachiliwa huru baada ya kukamatwa kwani wahasiriwa wachache ambao hupiga ripoti katika vituo vya polisi huwa hawafiki mahakamani kuhudhuria kesi hizo. 

Maafisa hao walinukuu mfano mmoja wa Wakenya ambao wameeleza wizi unaoendelea kwenye mitaa ya jiji kuu.

Jamaa kwa jina @MwendaChris alitahadhisha Wakenya dhidi ya kijia kinachotoka cha Standard street kutoka hoteli ya 680 kuelekea City Hall na jengo la mahakama ya kuu baada ya saa moja unusu.

Alieleza kuwa kuna genge la wahuni  4-6 ambalo lilikuwa likiwaibia watu pale huku akisema kuwa mmoja wao huwa amebeba kisu.

Mwenda alitahadharisha kuwa kuna magenge mengi  ambayo yanashambulia watu katika maeneo ya Kencom, kijia cha Aga Khan na karibu na mahakama kuu. Alisema kuwa alikuwa mhasiriwa wa wezi hawa ingawa alinusurika kifo.

"Ni bahati kufika nyumbani nikiwa mzima, jiji la Nairobi laweza kumaliza" Mwenda aliandika.

Wakenya wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya Twitter na Instagram kusimulia yaliyowapata mikononi mwa wezi jijini Nairobi na kuhamasisha wengine dhidi ya matendo yale.

Siku ya Jumatatu, Wakenya wenye ghadhabu walishambulia kikundi cha watu walioshukiwa kuwa watapeli katika eneo la Archives na kuharibu mali na gari lao.

Hapo awali, idadi kubwa ya Wakenya walikuwa wamezungumzia kikundi hicho kwenye mtandao wa Twitter wakieleza kuwa kilikuwa kinawashawishi watu kuwa wangeshinda kitu fulani wapo wangetoa kiwang fulani cha pesa.

Baada ya kuongelea genge hilo kwa muda, kikundi cha Wakenya kiliamua kuchukua sheria mikononi na kuwashambulia asubuhi ya Jumatatu.