Haki za Binadamu zinavyomtenganisha Rais Samia na utawala uliopita

Muhtasari

• Hali ilianza kubadilika kuanzia mwaka 2016 kutokana na namna mpya ya uongozi chini ya Rais John Magufuli. 

• Muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani, Rais Samia akafungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma.

Rais Samia Suluhu wa Tanzania
Rais Samia Suluhu wa Tanzania
Image: GOOGLE

Haki za binadamu zinatumika kupima ustaarabu wa jamii husika kwenye kujali na kuheshimu misingi ya utu na utawala. Kwa misingi hiyo Umoja wa Mataifa uliamua kwa makusudi kuja na azimio la kimataifa kuhusu haki za binadamu mwaka 1948 na mataifa mbalimbali wanachama ikiwemo Tanzania wakaziwekea utaratibu ukiwemo wa kisheria kuzilinda.

Kwa mfano, baada ya kupitishwa kwa Sheria Na. 7 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya mwaka 2001, Tanzania ikaanzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kama taasisi huru ya Serikali ambayo ni kitovu cha kukuza na kulinda haki za binadamu na wajibu na utawala bora nchini humo.

Kuzorota kwa haki za Binadamu Tanzania

Kati ya mwaka 2005 mpaka 2015, haki za binadamu hasa kwenye maeneo ya Uhuru wa habari na vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, usalama wa mali na watu pamoja na uhuru wa kusikilizwa na kukosoa ulikuwa unapiga hatua. Maeneo haya yalisaidia sana hata kuibuliwa kwa kashfa kubwa kubwa.

Kashfa ya wizi wa fedha za zaidi ya shilingi bilioni 133 kwenye akaunti ya madeni ya nje yaani EPA katika Benki Kuu ya Tanzania iliyowahusisha baadhi ya vigogo wa benki hiyo, wafanya biashara maarufu pamoja na maafisa wa serikali kuu pamoja pamoja na kashfa ya kampuni hewa ya kufua umeme ya Richmond iliyopelekea waziri mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa kujiuzulu nafasi hiyo, ni kashfa baadhi za mifano tajika.

Lakini hali ilianza kubadilika kuanzia mwaka 2016 kutokana na namna mpya ya uongozi chini ya Rais John Magufuli. Pengine alifanya sawa kutokana na sheria zilizopo lakini wapo waliotazama tofauti.

Jeshi la Polisi Tanzania lilikusanya jumla ya matukio 443 ya mauaji yanayotokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Jeshi la Polisi Tanzania lilikusanya jumla ya matukio 443 ya mauaji yanayotokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi.

Mwaka 2018 Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulieleza wazi kuhusu kuzorota kwa haki za kiraia na haki za binadamu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

"Serikali ya Marekani imesikitishwa sana na matukio ya mashambulizi yanayoshamiri na hatua za kisheria zinazochukuliwa na serikali ya Tanzania, ambazo zinakiuka uhuru wa raia na haki za binadamu, na zinazojenga mazingira ya vurugu, vitisho na ubaguzi. Tunahuzunishwa na hatua za ukamataji watu unaoendelea na unyanyasaji wa makundi maalum, wanaotaka kutumia haki zao za uhuru wa kujieleza, kushiriki na kukusanyika. Vyombo vya kisheria vinatumika kudhibiti uhuru wa raia kwa wote," Ilieleza sehemu ya taarifa ya ubalozi huo.

Mbali na ubalozi huu, ripoti mbalimbali za haki za binadamu ikiwemo kutoka shirika la kimataifa la Human Right Watch, Kituo cha sheria na Haki za binadamu nchini(LHRC), na mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, zote zilionyesha haki za binadamu zilivyo katika hali tete nchini Tanzania hasa kuanzia mwaka 2015, baada ya kuingia madarakani kwa utawala wa John Magufuli.

Kulishuhudiwa kuongezeka kwa vitendo vya kutekwa kwa watu, watu kubambikiwa mashtaka, kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari, kushambuliwa na kukamatwa kwa wanahabari, kushambuliwa na kupotea kwa watu hasa wakosoaji wa serikali, kuibuka kwa kundi la watu wasiojulikana wanaoshambulia na kukamata watu, kuminywa kwa uhuru wa kujieleza na kukosoa, kukandamizwa kwa asasi za kiraia kutekeleza wajibu wao pamoja na watuhumiwa kufia mikononi mwa dola.

Kwanini Samia anatazamwa kupita njia tofauti na mtangulizi wake?

Siku 100 si nyingi kumpima mtu hasa kiongozi wa nafasi kubwa kama ya Urais kwenye kusimamia na kutekeleza majukumu yake, lakini zinatosha sana kupima nia na dhamira yake hasa linapokuja suala la haki za binadamu. Ni rahisi kwa sababu ni haki ambazo kila mtu anapaswa kuwa nazo bila kujali cheo, jinsia, dini, rangi, taifa au tabaka lolote, ili mradi yeye ni binadamu basi haki hizo zinamuhusu. Kwa mfano haki ya kuishi, haki ya kuwa huru na usalama wako, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na haki dhidi ya ukatili.

Tangu aingie madarakani katika eneo hili la haki za binadamu Rais Samia ameonyesha uelekeo tofauti na mtangulizi wake, anaweza kutajwa kufanya vyema katika masuala manne muhimu ambayo ni haki na ambao mataifa ya nje, wanaharakati na hata wapinzani wa siasa za Tanzania, wanayaona kama masuala yanayomtofautisha Rais Samia na utawala uliopita.

Uhuru wa habari na Haki ya kupata taarifa

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali hali ya uhuru wa habari Tanzania imezidi kushuka katika nyanja za kimataifa. Kwa mujibu wa taarifa ya wandishi wa habari wasio na mipaka duniani, tangu mwaka 2016, uhuru wa habari Tanzania umekuwa ukishuka kila mwaka huu.

Mwaka 2016, kati ya mataifa 180, Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya 71, mwaka 2018 ilikua ya 83, mwaka 2019 ilishika nafasi ya 93 na mwaka 2020 imeshuka mpaka nafasi ya 123.

Lakini muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani, Rais Samia akafungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma na tayari wasaidizi wake wameeleza baadhi ya sheria mbalimbali zikiwemo zile zinazosimia habari zinaweza kupitiwa upya na kufanyiwa marekebisho.

Katika miaka sita iliyopita zipo sheria mbalimbali palishuhudiwa sheria kama ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na sheria ya upatikanaji wa habari ya mwaka 2016 zikipitishwa, ambazo baadhi ya wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu wanaziona kama zinakinza uhuru wa habari

Hatua ya kufungulia vyombo vya habari pekee imemtofautisha kimtazamo na mtangulizi wake, Rais Magufuli ambaye aliwaonya wanahabari kwamba vyombo vya habari vina uhuru lakini sio uhuru usio na mipaka.

Uhuru wa kujieleza na kukosoa

Wiki chache kabla hajafariki, Rais Magufuli wakati akifunguajengo la kituo cha Televisheni cha Channel Ten jijini Dar es Salaam, alieleza kwamba serikali yake haichukii kukosolewa, ila ukosoaji huo uwe wa staha.

' Serikali hatuchukii wanaotupa changamoto na kutukosoa kwa staha. Kitakwimu, tumeruhusu vyombo vingi sana vya habari katika kipindi hiki kuliko wakati wowote tangu tupate uhuru', alisema Magufuli.

Rais Samia amebeba kauli hii kwa vitendo, akilihutubia Bunge mjini Dodoma, mara baada ya kuapishwa kuwa Rais akaruhusu kukosolewa kwa lugha ya 'staha' lakini pia akizungumza na vijana jijini Mwanza aliwambia kwamba wanaweza kulaumu na kuikosoa serikali yake kwa kupitia mitandao lakini wafanye hivyo kwa kutoa na suluhisho pia.

Haki ya kuishi

Inaelezwa na ripoti ya haki za binadamu kwamba mwaka 2020, Jeshi la Polisi Tanzania lilikusanya jumla ya matukio 443 ya mauaji yanayotokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi.

Pamoja na mauaji haya, mauaji ya vikongwe, mashambulizi na mauaji ya madereva bodaboda na watuhumiwa kufia mikononi mwa jeshi la Paolisi, katika siku 100 za kwanza za Rais Samia, matukio haya hayajashuhudiwa kwa kiwango cha kuyazungumzia.

Rais Samia ameeleza wazi wasaidizi wake kufanya kazi kwa kuangalia haki za watu na bila kumuonea mtu.

'Hakuna kitu kikubwa amefanya zaidi ya kauli zake tu, husikii watu wakifanya mauaji ya wazi kama zamani, sasa ni kama watu wanaheshimu utu na haki za mtu kuishi, na ni rahisi uchumi kukua kama watu wana uhakika na uhai wao' Beatrice Kimaro, mchambuzi wa masuala ya uchumi na jamii.

Haki ya kuwa huru na salama

Kwa mujibu wa mikataba na maono ya wanaharakati wa haki za binadamu haki ya kuwa huru na salama ni haki ya msingi ya binadamu, ambayo inajumuisha uhuru dhidi ya ukamataji na uwekaji kuzuizini kinyume na sheria na haki ya dhamana.

Ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2020 iliyotolewa na LHRC na ripoti zingine za miaka 5 iliyopita ilonyesha haki hii iliendelea kuathiriwa na vitendo vya ukamataji na uwekaji kizuizini watu kwa muda mrefu kinyume na sheria; unyimaji wa dhamana; ubambikaji wa kesi; ucheleweshaji katika kufanya na kukamilisha uchunguzi wa kesi; na usafirishaji haramu wa binadamu.

Lakini katika siku 100 za Rais Samia, kumeshuhudiwa watu waliokuwa jela kwa muda mrefu kwa makosa mbalimbali wakianza kuachiwa wakiwemo Masheikh 36 wa kundi la kiislamu la mihadhara la Uamsho, wafanyabiashara kama Papa Msofe na watu wengine.

Hivi karibuni Mashekh 36 wa kikundi cha mihadhara ya kiislam cha Uamsho, walifutiwa mashitaka na kuachiwa huru baada ya kukaa jela miaka zaidi ya 7
Hivi karibuni Mashekh 36 wa kikundi cha mihadhara ya kiislam cha Uamsho, walifutiwa mashitaka na kuachiwa huru baada ya kukaa jela miaka zaidi ya 7
Image: GOOGLE

Kesi 147 za kubambikizwa zilifutwa mara moja na Taasisi ya kupambana kuzuia Rushwa (TAKUKURU), ikiwa ni muda mfupi baada ya Rais Samia kutaka Jeshi la Polisi kufuta kesi za aina hiyo ili kupunguza mlolongo wa mahabusu magerezaji.

Katika siku 100 za Rais Saia, hakuna mtu aliyetangazwa kupotea ama watu wasiojulikana kutajwa kuteka mtu yoyote. Kwa mujibu wa wanaharakati na wananchi wa kawaida, hiyo ni ishara ya kwamba Rais Samia hatamani kuona vitendo vya kutezwa utu na ukatili dhidi ya watanzania.

'Sasa najiona huru na niko salama sana, hata kama maisha yangu ni magumu sina pesa', lakini nina furaha na kauli tu za mama (Rais Smia) zinatia moyo', alisema Maulid Kasimu, mwendesha boda boda.

Hatua hii pekee inaonyesha nana anavyojipambanua kwenye kulinda haki ya watu ya kuwa huru na salama.

Wanaharakati wa haki za binadamu wanasemaje?

Anna Henga, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu nchini Tanzania (LHRC)
Anna Henga, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu nchini Tanzania (LHRC)
Image: LHRC

"Kwa sasa kuna haueni sana sana", anaanza kusema Anna Henga, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu nchini Tanzania (LHRC), ambao katika utawala uliopita, waliwahi kuvamiwa na Jeshi la Polisi, huku afisa wake Tito Magoti akiwekwa ndani kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kutolewa hivi karibuni kwa utaratibu wa Plea Bargain' unaosimamiwa na mwendesha MASHTAKA (DPP). Kadhia hiyo iliukumba pia Mtandao wa kutetea haki za binadamu nchini Tanzania (THRDC).

Khisah Gohagi kutoka Binti Makini anasema ni wakati wa kufurahia kwa kuwa haki za binadamu kwa sasa nchini Tanzania zimekuwa zikiheshimiwa na kulindwa.

Ingawa wapo wanaoona kwamba ni mapema mno kumpigia chapuo Rais Samia kwamba amefanya vizuri kwenye kusimamia na kuheshim haki za binadamua, lakini kwa mwanaharakati Anna Henga anasema hata kama sheria na kanuni hazijabadilika, lakini haki za binadamu zinaonekana kuheshimiwa na kulindwa tofauti na nyuma lakini hoja yake kubwa ni kwamba, "wasaidizi wake watamuunga mkono?".

Hilo ni swali ambalo wengi wanajiuliza, inawezekana Samia kaanza na mguu wa kulia kwenye haki za binadamu, lakini wasaidizI wake wakiwemo mawaziri, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na Jeshi la Polisi watazungumza lugha moja? Ni jambo la kutoa muda na kuona.