Kaunti zapokea bilioni 43.5; Yatani ashauri magavana kulipa madeni kwanza

Yatani ameahidi kuwa fedha za Mei na Juni zitalipwa hivi karibuni

Muhtasari

•"Uchumi unapoendelea kufanya vizuri haswa katika ukusanyaji wa mapato, hazina ya kitaifa itaendelea kupea kipaumbele kulipa madeni ya mwezi wa Mei na Juni." Yatani alisema.

•Haya yanajiri wiki moja tu baada ya baraza la magavana kutishia kusimamisha shughuli za kaunti kuanzia tarehe 24 Juni kufuatia ukosefu wa fedha.

Ukur Yatani
Ukur Yatani
Image: Maktaba

Kaunti zimepokea bilioni 43.5 kutoka kwa hazina ya kitaifa.  Waziri wa hazina, Ukur Yatani ametangaza kuwa pesa hizo zimelipwa kwa akaunti za kaunti mnamo Juni 23.

Kupitia ujumbe kwa wanahabari, Yatani ameshauri serikali za kaunti  kutumia fedha hizo kulipa deni walizo nazo kwa wasambazaji bidhaa na madeni mengine ya dharura.

Kulingana na ujumbe huo,  malipo hayo yatafuatiliwa kwa karibu na hazina ya kitaifa huku kaunti zikiahidiwa kuwa  malipo ya fedha za mwezi Mei na Juni yatapewa kipaumbele.

"Uchumi unapoendelea kufanya vizuri haswa katika ukusanyaji wa mapato, hazina ya kitaifa itaendelea kupea kipaumbele kulipa madeni ya mwezi wa Mei na Juni." Yatani alisema.

Haya yanajiri wiki moja tu baada ya baraza la magavana kutishia kusimamisha shughuli za kaunti kuanzia tarehe 24 Juni kufuatia ukosefu wa fedha.

Mwenyekiti wa baraza la magavana Martin Wambora alilalamikia kucheleweshwa kwa fedha hizo huku akisema kuwa shughuli za kaunti zilikuwa zimelemazwa. Alisema kuwa hazina ya kitaifa ilikuwa na deni ya bilioni 102.6 kwa kaunti.

“Iwapo hazina ya kitaifa haitawachilia pesa , kaunti hazitaweza kupeana huduma za kimsingi na kwa hivyo italazimu kusimamishwa kwa huduma ama kufungwa kabisa kwa kaunti kuanzia Juni 24 Wambora alisema.

Magavana walikuwa wamepatia hazina ya kitaifa hadi Alhamisi wiki kutuma pesa hizo kwa akaunti za kaunti