Mahakama yaidhinisha kuteuliwa kwa Ann Kananu kama naibu gavana

Muhtasari
  • Pigo kwa Sonko baada ya korti kuamua uteuzi wa kananu na kuapishwa kama naibu gavana ulifanywa kulingana na sheria
Anne Kananu akiapishwa naibu gavana wa Nairobi, Januari 15, 2021.
Anne Kananu akiapishwa naibu gavana wa Nairobi, Januari 15, 2021.
Image: EZEKIEL AMINGA

Korti Kuu mnamo Alhamisi iliamua kwamba uhakiki wa uteuzi na kuapishwa kwa Anne Kananu kama Naibu Gavana ulifanywa kulingana na sheria.

Benchi la majaji watatu lililotoa uamuzi huo liliongozwa na Jaji Said Chitembwe na kusaidiwa na Majaji Wilfrida Okwany na Weldon Korir.

Hata hivyo, Jaji Korir hakuwepo kortini wakati wa uamuzi huo.

Jaji Chitembwe alisema Jaji Korir alipata dharura lakini akasaini uamuzi huo ambao unakubaliana.

Korti ilisema kwamba kabla ya kushtakiwa, Sonko alimchagua Kananu kama naibu gavana na kwa uteuzi huo, mamlaka yake iliishia hapo.

"Hatupati kosa katika bunge la kaunti kumchunguza Kananu," Okwany alisema.

Korti iliamua kwamba kulikuwa na ushiriki unaofaa wa umma katika ukaguzi wa Kananu ukipuuza hoja za Sonko kwamba hakuna ushiriki wa umma.

"Bunge la kaunti lilifuata mahitaji ya ushiriki wa umma katika kukagua Kananu," Okwany alisema.

Korti ilitupilia mbali hoja kwamba Kananu alipaswa kuteuliwa rasmi afisini baada ya kuchunguzwa na Sonko na sio kaimu gavana.

Korti iliamua kwamba kaimu gavana anaweza kumaliza mchakato wa kuapishwa kwake na kwamba hakuna chochote kibaya kwa kuapishwa kwa Kananu.

"Kama Kananu angekaguliwa kabla ya kumshtaki Sonkos basi angekuwa Naibu Gavana. Kuchunguzwa kwa Kananu kabla ya mashtaka yake hakuwezi kufutwa," Okwany alisema.

"Spika aliruhusiwa na sheria kuleta mchakato huo wa uteuzi wa Kananu utimie.

Ingawa spika anayefanya kazi kama gavana hana uwezo wa kuteua naibu gavana, kesi hii ilikuwa tofauti kwa sababu tayari kulikuwa na naiu gavana aliyeteuliwa."

Korti iliamua kuwa walikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo linalohusu uteuzi wa Naibu Gavana Anne Kananu.

Sonko na waombaji wengine wote walikuwa wamepinga uteuzi wake wakisema ni kinyume cha sheria.

Sonko alisema alikuwa amebatilisha uteuzi wake mnamo Desemba 2020.

Hata hivyo, Kananu alikuwa amesema kuwa kuondolewa kwa uteuzi wake na Sonko kulikuwa na nia mbaya.

Korti iligundua kuwa Sonko hakuwahi kuondoa uteuzi wa Kananu kama naibu gavana kama vile alidai.