Mashindano ya WRC Safari Rally yatakuwa yakifanyika nchini kila mwaka hadi 2026, Rais Kenyatta atangaza.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa Kenya imepata idhini ya kufanya mashindano hayo kutoka kwa shirika la World Rally Championship(WRC) na International Automobile Federation(FIA).

Muhtasari

•Ushindi wa mashindano hayo ambayo yalifanyika nchini kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 19 iliyopita ulinyakuliwa na Mfaransa Sebastian Ogier akifuatwa na Takamoto Kasutsa wa Ujapani.

•Rais Kenyatta alisema kuwa serikali itaanza mikakati ya kujiandaa kwa mashindano yatakayofanyika mwaka ujao.

Rais Kenyatta akizungumza kwenye hafla ya kutunza washindi wa WRC Safari Rally siku ya Jumapili
Rais Kenyatta akizungumza kwenye hafla ya kutunza washindi wa WRC Safari Rally siku ya Jumapili
Image: Hisani

Hatimaye  mashindano ya magari ya WRC Safari Rally 2021 yalitamatika Jumapili baada ya siku tatu za msisimko na burudani si haba.

Ushindi wa mashindano hayo ambayo yalifanyika nchini kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 19 iliyopita ulinyakuliwa na Mfaransa Sebastian Ogier akifuatwa na Takamoto Kasutsa wa Ujapani.

Habari njema ni kuwa mashindano hayo ambayo yalifanyika tena nchini kwa mara ya mwisho mwaka wa 2002 yataendelea kufanyika nchini kila mwaka hadi mwaka wa 2026.

Akizungumza baada ya kutamatika kwa mashindano hayo siku ya Jumapili, rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa Kenya imepata idhini ya kufanya mashindano hayo kutoka kwa shirika la  World Rally Championship(WRC) na International Automobile Federation(FIA).

"Inanipa raha kutangaza kuwa tumekubaliana na FIA na WRC kuendelea kuwa na mashindano ya magari nchini kila mwaka hadi 2026" Rais alisema.

Alisema kuwa serikali itaanza mikakati ya kujiandaa kwa mashindano yatakayofanyika mwaka ujao.

"Serikali yangu itaanza kujiandaa kwa hafla ya mashindano hayo ambayo itafanyika mwaka ujao. Naahidi kupatiana fedha zote zitakazohotajika ili kufanikisha mashindano mengine nchini Kenya" Uhuru alisema.

Kufuatia kufanikiwa kwa  mashindano ambayo yalitamatika, rais alisema kuwa Kenya imeonyesha ulimwengu kuwa ilikuwa tayari kuwa mwenyeji wa mashindano ya kidunia licha ya janga la Korona.

Alikumbusha wa Kenya kuwa ahadi yake ya kurejesha WRC Safari Rally nchini ambayo alitoa mwaka wa 2013 ilikuwa imetimia.

Rais pia aliwapongeza wote ambao walishiriki kwenye mashindano hayo na kuwapa motisha madereva ambao hawakufanikiwa kutia bidii ili kupata matokeo bora kwenye mashindano yajayo.

Aliwatakia kupona kwa haraka wale ambao waliumia kwenye mashindano hayo kama vile Tajveer Rai wa Kenya miongoni mwa wengine.

Onkar Rai ambaye ni ndugu ya Tajveer aliyeumia siku ya kwanza ya mashindano hayo aliibuka dereva bora kutoka Kenya baada ya kushinda mashindano ya siku ya Jumapili na  kuibuka nambari saba. Alikuwa akisaidiana na Drew Sturrock.

Rais alikuwa akizungumza Jumapili katika kituo cha mafunzo cha Kenya Wildlife Service Training Institute (KWSTI) wakati ambao alikuwa anatunza washindi wa mashindano hayo.

Viongozi wengine ambao walihudhuria ni pamoja na Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, waziri Najib Balala na Amina Mohammed.