Kenya itawekeza shilingi bilioni 2.5 kuimarisha vita dhidi ya dhuluma za kijinsia- Rais Kenyatta

Rais alisema kuwa kesi za dhuluma ya kijinsia zimeongezeka barani Afrika hadi kiwango kinachohitaji suluhu ya dharura.

Muhtasari

•Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa serikali itawekeza shilingi bilioni 2.4 kwenye vita dhidi ya dhuluma ya kijinsia kufikia mwaka wa 2022. Kenyatta amesema kuwa kiwango hicho cha fedha kitaongezwa hadi bilioni 5.4 kufikia mwaka wa 2026 ili kuimarisha vita hiyo.

•Alisema kuwa bara Afrika limeshuhudia ongezeko ya shida hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja ambao umepita. Alitaja kuwa Kenya(50%), Liberia(50%), Central Afrika Republic(50%), Afrika Kusini(37%) na Cameroon(35%) ndiyo mataifa amabyao yamerekodi ongezeko kubwa zaidi ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Rais Uhuru Kenyatta akizungumza katika mkutano wa kijinsia jijini Paris, Ufransa siku ya Jumatano
Rais Uhuru Kenyatta akizungumza katika mkutano wa kijinsia jijini Paris, Ufransa siku ya Jumatano
Image: Hisani//PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa serikali itawekeza shilingi bilioni 2.4 kwenye vita dhidi ya dhuluma ya kijinsia kufikia mwaka wa 2022.

Kenyatta amesema kuwa kiwango hicho cha fedha kitaongezwa hadi bilioni 5.4 kufikia mwaka wa 2026 ili kuimarisha vita hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa usawa wa kijinsia jijini Paris, Ufaransa siku ya Jumatano, rais alitangaza kuwa kesi za dhuluma ya kijinsia zimeongezeka barani Afrika hadi kiwango kinachohitaji suluhu ya dharura.

Rais ambaye ako katika ziara ya kiofisi ya siku mbili nchini Ufaransa alisema kuwa janga la Corona limechangia kuongezeka kwa kesi hizo kote duniani. Kufuatia ongezeko ya kesi hizo, Kenyatta ametoa wito kwa mataifa yote kufanya dharura kutafuta suluhu ya dhuluma hizo.

"COVID 19 imechangia kuongezeka kwa hali hii na ikafanya dhuluma za kijinsia kuwa jambo la dharura.. Ripoti za hivi sasa zinaashiria kuwa kuna ongezeko ya angalau asilimia 25% ya dhuluma dhidi ya wanawake kote duniani" Rais Kenyatta alisema.

Kiongozi huyo wa taifa aliandamana na waziri wa maswala ya nje, Raychelle Omamo, waziri wa barabara na miundombinu James Macharia na waziri wa jinsia Margaret Kobia  na anatarajiwa kushiriki mazungumzo na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Kenyatta alisema kuwa dhuluma ya kijinsia ni tatizo ambalo linadhuru zaidi ya asilimia 36% ya wanawake ambao wako na umri wa kati ya miaka 15-49.

Alisema kuwa bara Afrika limeshuhudia ongezeko ya shida hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja ambao umepita. Alitaja kuwa Kenya(50%), Liberia(50%), Central Afrika Republic(50%), Afrika Kusini(37%) na Cameroon(35%) ndiyo mataifa amabyao yamerekodi ongezeko kubwa zaidi ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Rais alisema kuwa Kenya inajitahidi kumaliza kesi za dhuluma ya kijinsia kufikia mwaka wa 2030.

"Kenya imefanya juhudi kubwa kusuluhisha tatizo la dhuluma za kijinsia. Nimejitolea kumaliza ukeketaji wa wanawake katika muhula wangu uongozini na kumaliza dhuluma zozote za kijinsia kufikia 2030" Kenyatta alisema.

Alisema kuwa nchi ya Kenya inapanga kuweka na kutekeleza sheria na sera za kukabiliana na tatizo la dhuluma za kijinsia.