Dereva afariki, wawili wajeruhiwa vibaya baada ya lori ya maji kuanguka shimoni Machakos

Dereva aliaga hapo hapo baada ya lori ya maji ambayo alikuwa akiendesha kupoteza mwelekeo barabarani na kuanguka ndani ya shimo kubwa mida ya saa nne na dakika ishirini.

Muhtasari

•Kamanda wa polisi eneo la Athi River, Anderson Njagi alisema kuwa lori hilo lilipoteza mwelekeo na kuanguka ndani ya shimo ambalo lilikuwa chimbo ya mawe lililo upande wa Mlolongo.

Wakazi wazingira lori ya maji iliyoanguka shimoni baada ya kupoteza mwelekeo maeneo ya Athi River
Wakazi wazingira lori ya maji iliyoanguka shimoni baada ya kupoteza mwelekeo maeneo ya Athi River
Image: GEORGE OWITI

Habari na George Owiti

Mwanaume mmoja alifariki Jumanne asubuhi baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya maeneo ya Mlolongo, kaunti ya Machakos.

Elijah Juma aliaga hapo hapo baada ya lori ya maji ambayo alikuwa akiendesha kupoteza mwelekeo barabarani na kuanguka ndani ya shimo kubwa  mida ya saa nne na dakika ishirini.

Kamanda wa polisi eneo la Athi River, Anderson Njagi alisema kuwa lori hilo lilipoteza mwelekeo na kuanguka ndani ya shimo ambalo lilikuwa chimbo ya mawe lililo upande wa Mlolongo.

Njagi alisema kuwa dereva wa gari hilo alikufa papo hapo na abiria wengine wawili wakanusurika na majeraha mabaya mwilini.

Alisema kuwa Benjamin Mwova, 27, na Kennedy Ireri, 30, walikimbizwa katika hospitali ya Assis Nursing Home.

Mwili wa dereva huyo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Shalom. Lori iliyohusika kwenye ajali hiyo ilipelekwa katika kituo cha polisi cha Athi River.

Uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo umeanza.

Njagi aliwaonya waendesha magari kuwa makini barabarani ili kuzuia ajali kama ile.