Kampuni ya Sputnic yadai fidia ya bilioni 4.8 kutoka kwa NMG

Kampuni hiyo iliingia tena makubaliano ya usambazaji na Harleys Limited, msambazaji wa dawa nchini Kenya

Muhtasari

• Dinlas Pharma EPZ Limited inadai kwamba imepata hasara ya dola milioni 45 (Sh4.8 bilioni), kufuatia chapisho la 'COVID Millionaires' katika jarida la kila siku.

• Kampuni hiyo iliingia mkataba wa kuagiza chanjo ya Sputnik V kutoka Urusi kupitia Dubai. Uingizaji ulipaswa kuwa katika makasha mawili ya dozi 75,000 na milioni 1.

LIPA NA UKOME: Wakili Donald Kipokorir
LIPA NA UKOME: Wakili Donald Kipokorir
Image: MAKTABA

Taarifa ya Susan Muhindi 

Kampuni iliyoingiza nchini chanjo ya Covid-19 ya Urusi ya Sputnik V imeishtaki kampuni ya Nation Media Group ikitaka fidia ya shilingi bilioni 4.8 kwa kupoteza biashara.

Kampuni hiyo inataka korti iamuru NMG iwalipe ada ya kufungua faili mahakamani na izuiliwe kuchapisha taarifa ambazo zinadhalilisha kampuni hiyo.

Dinlas Pharma EPZ Limited inadai kwamba imepata hasara ya dola milioni 45 (Sh4.8 bilioni), kufuatia chapisho la 'COVID Millionaires' katika jarida la kila siku linalomilikiwa na kampuni ya NMG.

Dinlas inasema kutokana na chapisho sifa yake ya biashara imeharibiwa sana na kuingizwa kwenye kashfa ya umma.

Kupitia wakili Donald Kipkorir, kampuni hiyo ilitoa ilani ya makataa kutaka kusitishwa kwa chapisho lolote dhidi ya Dinlas mnamo Aprili 7 kwa NMG lakini wamekataa na kupuuza kujibu.

"Tuna hofu kwamba wasipozuiwa washtakiwa wataendelea kuchapisha maneno yale yale au yanayofanana," Dinlas Pharma EPZ Limited ilisema.

Dinlas iliingia mkataba wa kuagiza chanjo ya Sputnik V kutoka Urusi kupitia Dubai. Uingizaji ulipaswa kuwa katika makasha mawili ya dozi 75,000 na milioni 1.

Kampuni hiyo iliingia tena makubaliano ya usambazaji na Harleys Limited, msambazaji wa dawa nchini Kenya.

"Tuliomba na kupokea idhini zote za uagizaji uliotajwa," inasema.

Kulingana na hati za mahakama, chapisho la Aprili 2 lilileta dhana kuwa Dinlas ni kampuni fisadi inayokusudia kulaghai umma.

Dinlas wanasema maneno hayo yaligusia sakata ya Kemsa, inayochunguzwa na Bunge na kwamba iliingiza Sputnik V bila idhini ya shirika la afya duniani WHO.