Spika Lusaka akubali ndiye baba wa mtoto wa mwanamke aliyemshtaki, aomba kesi kusuluhishwa nje ya koti

Lusaka amearifu mahakama kuwa kesi kuhusu ulezi wa mtoto huyo inafaa kushughulikiwa katika mahakama ya watoto ndani ya kipindi cha miezi saba baada ya mtoto kuzaliwa.

Muhtasari

•Kupitia wakili wake Peter Wanyama, Lusaka ameambia koti kuwa amekuwa kwenye mazungumzo na mwanamke huyo wakilenga kusuluhisha kesi nje ya mahakama.

•Wakili Wanyama alisema kuwa Lusaka ako tayari kugharamia bili zote za hospitali ambazo zitakuwepo kabla ya mwanamke huyo kujifungua.

Senate speaker Kenneth Lusaka
Senate speaker Kenneth Lusaka
Image: EZEKIEL AMINGA

Habari na Annette Wambulwa

Spika wa seneti Kenneth Lusaka ameambia mahakama kuwa hana nia ya kupinga kesi ya kuwa  baba wa mtoto wa  mwanamke aliyemshtaki wiki mbili zilizopita.

Kupitia wakili wake Peter Wanyama, Lusaka ameambia koti kuwa amekuwa kwenye mazungumzo na mwanamke huyo wakilenga kusuluhisha kesi nje ya mahakama.

Hata hivyo, amearifu mahakama kuwa kesi kuhusu ulezi wa mtoto huyo inafaa kushughulikiwa katika mahakama ya watoto ndani ya kipindi cha miezi saba baada ya mtoto kuzaliwa.

Wakili Wanyama alisema kuwa Lusaka ako tayari kugharamia bili zote za hospitali ambazo zitakuwepo kabla ya mwanamke huyo kujifungua.

Wakili Danstan Omari ambaye anawakilisha mwanamke huyo amethibitisha kuwa ni kweli wamekuwa wakipatana na kujadiliana kuhusiana na suala hilo na wanahitaji siku saba kutamatisha majadiliano.

Wanyama aliambia mahakama kuwa Omari na yeye walihudhuria mkutano ambao Lusaka na mwanamke huyo walikuwepo.

"Si kweli kuwa mteja wangu hawezi gharamia matumizi ya ujauzito . Hiyo ni suala ndogo na imetatuliwa" Wanyama alisema.

Wanyama alisema kuwa sababu Omari anataka kuharakisha suala hilo ni ili  kumshinikiza Lusaka kwani wanataka awanunulie  nyumba  ndani ya kipindi cha siku saba zijazo. Alitaka kujua kwa nini hawawezi  subiri mtoto azaliwe ili watafutiwe mahali pazuri pa kukaa na gharama zingine.

Omari kwa upande wake alisema kuwa siku 30 ni nyingi kwa hali ambapo Lusaka amekubali ndiye baba ya mtoto na kusihi mahakama ikubali siku 7 kwani maisha ya mtoto yule ambaye hajazaliwa yamo hatarini.

Jaji Mrima aliruhusu pande hizo mbili kuendelea na mazungumzo na kusema kuwa kesi hiyo itatajwa mnamo Julai 28 kwa maelekezo zaidi.