Kenya yapokea msaada wa dozi 182,400 za chanjo aina ya AstraZeneca kutoka Ufaransa

Chanjo hizo ambazo zilisafirishwa na UNICEF ziliwasili katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta Alhamisi asubuhi.

Muhtasari

•Akhwale alisema kuwa chanjo hizo zitahakikisha kuwa wahudumu wa afya, waalimu na watu wanaotoa huduma muhimu wamezuiliwa kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Dozi 182,400 za chanjo ya Corona zawasili JKIA Alhamisi asubuhi
Dozi 182,400 za chanjo ya Corona zawasili JKIA Alhamisi asubuhi
Image: UNICEF

Kenya imepokea msaada wa dozi  182,400 za chanjo ya Corona aina ya AstraZeneca-Oxford kutoka Ufaransa.

Chanjo hizo ambazo zilisafirishwa na UNICEF ziliwasili katika uwanja wa ndege  wa Jomo Kenyatta Alhamisi asubuhi.

Zilipokewa na baadhi ya maafisa wa wizara ya afya nchini, mshauri wa masuala ya siasa nchini Ufaransa Emmanuel Dagron na mwakilishi wa UNICEF, Maniza Zaman.

Mwenyekiti wa kamati ya kusambaza chanjo ya COVID 19, Willis Akhwale alishukuru serikali  ya Ufaransa kwa niaba ya serikali ya Kenya.

"Serikali ya Kenya inashukuru serikali ya Ufaransa kwa msaada wa kikarimu ambao utasaidia katika shughuli ya kupeana chanjo nchini" Akhwale alisema.

Akhwale alisema kuwa chanjo hizo zitahakikisha kuwa wahudumu wa afya, waalimu na watu wanaotoa huduma muhimu wamezuiliwa kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Emmanuel Dagron ambaye alizungumza kwa niaba ya balozi wa Ufaransa nchini Kenya na Somalia, Aline Kuster-Menager alisema kuwa Ufaransa, Jumuiya ya Ulaya na COVAX wako makini kufanya kazi na serikali ya Kenya katika juhudi yake kukabiliana na virusi vya Corona.

"Tunatumai kuwa dozi hizi 182,400 zitasaidia Wakenya walio hatarini kubwa kupata dozi ya pili ya chanjo." Dagron alisema.

Rais Macron wa Ufaransa aliahidi kupeana dozi 60,000,000 kwa mataifa mbalimbali kote duniani ikiwemo Kenya kufikia mwisho wa mwaka wa 2021. 

Kufikia mwisho wa Juni, dozi milioni 2.6  zimesambazwa katika mataifa mbalimbali.