Kwa nini polisi mwanamke anayesakwa nchini Kenya anawaua wanaume?

Muhtasari

• Caroline Kangogo, aligonga vichwa vya habari kwa kumuua polisi mwenzake John Ogweno, mjini Nakuru.

• Kilomita 200 kutoka eneo la tukio la kwanza polisi huyo alimuua kwa kumpiga risasi mwanaume mwingine Peter Njiru mwenye umri wa miaka 32 .

• Kinachofahamika ni kwamba hadi sasa ni kwamba anawalenga wanaume.

Image: DCI/KENYA

Polisi nchini Kenya wameanzisha msako mkubwa kumkamata mwenzao wa kike anayedaiwa kuwaua watu wawili-wanaume,baada ya kuwapiga risasi akiwemo afisa mwenzake wa polisi mwanzoni mwa wiki hii .

Polisi huyo wa kike aliyetajwa kama Koplo Caroline Kangogo, aligonga vichwa vya habari kwa kumuua polisi mwenzake aliyetambuliwa na idara ya jinai nchini humo kama John Ogweno, katika mji wa Nakuru.

Kilomita 200 kutoka eneo la tukio la kwanza polisi huyo alimuua kwa kumpiga risasi mwanaume mwingine Peter Njiru mwenye umri wa miaka 32 .

Hali inayozingira mauaji ya wawili hao ni ya kutatanisha kwani hakuna aliye na uhakika kabisa wa kiini cha mauaji yao.

Kinachofahamika ni kwamba hadi sasa ni kwamba anawalenga wanaume.

Taarifa iliyotolewa na polisi wakitangaza kumsaka mwenzao ni kama simulizi katika filamu ya kuogofya -ila tofauti ni kwamba haya sio maigizo bali tishio la kiusalama ambalo limewatia wengi hofu na kuna ripoti kwamba baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu polisi wamekimbia kwenda mafichoni baada ya Kagongo kuwatumia jumbe za kuwatisha kwamba anawalenga .

Yote yalianzaje?

Kangogo anashukiwa kumuua polisi mwenzake siku ya jumatatu katika mji wa Nakuru . Baada ya kumuua inadaiwa aliichukua bastola yake aina ya Ceska iliyokuwa na risasi .

Alielekea eneo la Juja ,kilomita 200 kutoka mji wa Nakuru ambako alilipia chumba cha kulala katika hoteli moja ambapo alimhadaa mwathiriwa wake wa pili Peter Njiru na walipokuwa chumbani humo alimpiga risasi kichwani.

Baadaye usiku wa manane aliondoka kutoka chumba hicho na kutoroka akiuacha mwili wa mwanaume huyo uliojaa damu kitandani .

Alimwambia mhudumu katika chumba hicho cha malazi kwamba alikuwa ameenda kununua dawa ya meno. Kangogo hakurudi.

Image: DCI/KENYA

Ogweno alipigwa risasi upande wa kulia wa kichwa na akavuja damu hadi kufa. Ganda la risasi lilipatikana katika eneo la tukio.

Jiwe lililotumiwa kuvunja dirisha la gari na kipande cha chuma pia vilipatikana na vitatumiwa kama ushahidi .

'Hatari na amejihami'

Polisi wamekuwa na wakati mgumu kujua aliko kwa sababu aliiacha simu yake katika eneo la kwanza alikotekeleza mauaji .

Kinachoshangaza mamlaka ni kwamba anatumia risasi moja kwa wahasiriwa wake, na amejihami na bastola iliyoibiwa iliyo na risasi 14.

Mkurugenzi wa idara Jinai George Kinoti alitoa wito kwa umma kuwasaidia kumkamata mwanamke huyo ambaye alimtaja kuwa "Sugu, aliyejihami na hatari".

Image: DCI/KENYA

Kangogo amehudumu katika vituo mbali mbali vya polisi, pamoja na kitengo cha polisi wa Reli, kabla ya kupelekwa Nakuru, ambapo amekuwa akifanya kazi kwa karibu miaka mitatu.

Kinoti alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akikwepa mtego wao tangu mapema Jumatatu .

"Tunaonya wananchi , haswa wanaume, kuchukua tahadhari dhidi ya afisa huyo mwovu ambaye anawashawishi wanaume katika mtego wake kabla ya kuwaua kikatili," alisema.