Nyumba ya mchambuzi wa siasa Mutahi Ngunyi yateketea katika hali tatanishi

Dakika 16 baada ya kuibuka kwa moto huo, mwahabari na msemaji wa 'Hustler Nation' Dennis Itumbi alitangaza mitandaoni habari kuhusu moto

Muhtasari

•Kulingana na mchambuzi huyo ambaye anajihusisha sana na mrengo unaounga rais Kenyatta mkono, nyumba yake iliyo maeneo ya Runda iliteketea mida ya saa nane kasorobo usiku.

•Itumbi alikuwa ameandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akiwaomba wazimamoto kukimbia na kusaidia kuzima moto ule.

Image: HISANI

Moto mkubwa uliteketeza nyumba ya mchambuzi wa siasa maarufu nchini, Mutahi Ngunyi  usiku wa kuamkia Jumatano. 

Kulingana na mchambuzi huyo ambaye anajihusisha sana na mrengo unaounga rais Kenyatta mkono, nyumba yake iliyo maeneo ya Runda iliteketea mida ya saa nane kasorobo usiku.

Hata hivyo hakusema kilichosababisha mkasa huo ulioharibu nyumba ambayo amemiliki kwa kipindi cha miaka 27.

Kabla ya Ngunyi kuthibitisha habari za mkasa huo, mwahabari na msemaji wa 'Hustler Nation' Dennis Itumbi alikuwa ametangaza mitandaoni  kuhusu moto huo  takriban dakika 16 baada ya kuibuka.

Itumbi alikuwa ameandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akiwaomba wazimamoto kukimbia na kusaidia kuzima moto ule.

"Wazimamoto tafadhali fanyeni hara mkaokoe nyumba ya Mutahi Ngunyi iliyo Runda. NMS harakisheni mkasaidie jamaa ambaye anawaunga mkono. Natumai ako salama na familia yake pia iko sawa. Kando na ujumbe wangu, naweza omba tu usiende hasara kubwa na uwe salama." Itumbi aliandika kwenye mtandao wa Twitter

Ngunyi alionekana kutilia shaka jambo hilo kwani kulingana na yeye, moto huo uliibuka dakika 16 pekee kabla ya Itumbi kutangaza habari hizo na awali siku hiyo alikuwa amezungumzia swala la vurugu zilizojitokeza maeneo ya Kiambaa mwaka wa 2008 kwenye stesheni yake ya 5th Estate.

"Rafiki yangu Ole Itumbi, nyumba yangu iliyo Runda  ya miaka 27 ilteketea 1.45AM. Uliambia Hustlers 2.01AM, takriban dakika 16 baadae. Hii ni baada yangu kuzungumzia vurugu zilizojitokeza Kiambaa mwaka wa 2008 kwenye runinga ya 5th Estate." Ngunyi aliandika.

Hata hivyo, Itumbi alijibu kuwa ujumbe wa Ngunyi yalikuwa ya kitundu.