SIASA ZA 2022

Siasa, mvutano, propaganda na malalamiko yashamiri Kiambaa

Kiongozi wa wengi bungeni, Amos Kimunya alijipata pabaya mapema leo alipokabiliana na kikundi cha vijana wanaounga mkono anayepeperusha bendera ya UDA wakidai kuwa mbunge huyo alikuwa na nia mbaya

Muhtasari

·Kiti cha ubunge maeneo ya Kiambaa kiliachwa wazi baada ya Koinange kuaga dunia mwishoni mwa mwezi Machi. 

•Mgombea kiti na tikiti ya UDA, John Njuguna alieleza ghadhabu yake kuhusiana na tukio hilo huku akisema kuwa kulikuwa na makubaliano kuwa hakuna mwanasiasa ambaye ataruhusiwa kufika katika vituo vya kupigia kura.

John Njuguna Wanjiku na Kariri Njama
John Njuguna Wanjiku na Kariri Njama
Image: HISANI

Hatimaye shughuli ya kuamua atakayeridhi kiti cha aliyekuwa mbunge wa Kiambaa marehemu Paul Koinange imeng'oa nanga.

Kiti cha ubunge maeneo ya Kiambaa kiliachwa wazi baada ya Koinange kuaga dunia mwishoni mwa mwezi Machi. 

Kufuatia hayo, IEBC ilitangaza kuwa uchaguzi mdogo ungefanyika mnamo tarehe 15 mwezi wa Julai. 

Farasi wakuu kwenye uchaguzi huo ni pamoja na John Njuguna Wanjiku wa chama cha UDA na Kariri Njama wa chama cha Jubilee.

Njama anaungwa mkono na wanaoegemea mrengo wa rais Uhuru Kenyatta huku Njuguna akipigiwa debe na wafuasi wa naibu rais William Ruto.

Kampeni za kuwania kiti hicho zilikuwa zimenoga huku wachambuzi wa siasa wakisema kuwa matokeo ya uchaguzi huo yatakuwa kielelezo muhimu cha uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Pande zote mbili zimetia bidii kupigia debe mgombea kiti wao huku matusi, malalamiko, propaganda na mvutano mkubwa ukishuhudiwa.

Kiongozi wa wengi bungeni, Amos Kimunya alijipata pabaya mapema leo alipokabiliana na kikundi cha vijana wanaounga mkono anayepeperusha bendera ya UDA wakidai kuwa mbunge huyo alikuwa na nia mbaya.

Vijana hao walimshambulia Kimunya alipoonekana katika kituo cha kupiga kura cha Kimuga na kumtaka aende huku wakidai kuwayeye sio ajenti rasmi au mpiga kura maeneo hayo.

Mgombea kiti na tikiti ya UDA, John Njuguna alieleza ghadhabu yake kuhusiana na tukio hilo huku akisema kuwa kulikuwa na makubaliano kuwa hakuna mwanasiasa ambaye ataruhusiwa kufika katika vituo vya kupigia kura.

"Tulikuwa na mkutano jana katika kituo cha kuhesabu kura cha Karuri na sote tukakubaliana pamoja na maafisa wanaosimamia uchaguzi kuwa hakuna mbunge atakayeruhusiwa kutembea tembea katika vituo vya kupigia kura. Kimunya alikuja hapa mapema sana asubuhi akiandamana na maafisa wa usalama" Njuguna alisema.

Uvumi ulikuwa umeenezwa mitandaoni kuwa mgombea kiti na tikiti ya Jubilee, Kariri Njama alikuwa amejiondoa kutoka kwenye kinyang'anyiro hicho.

Hata hivyo, kulingana na ujumbe ambao ulitolewa na chama hicho jioni ya Jumatano, madai hayo yalikuwa propaganda tu na hakukuwa na nia yoyote ya Njama kujiondoa.

"Mgombeaji wa Jubilee Kariri Njama ako ndani kabisa ya kinyanganyiro cha Kiambaa. Aibu sana kwa wapinzani ambao wamehisi kuwa watashindwa na wakaamua kutumia njia za kueneza  habari za uongo ambazo zilitumika 1960s" Katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alisema.

Mvutano mkubwa umeendelea kushuhudiwa katika maeneo hayo huku malalamiko mengi yakishuhudiwa, mengine ya kikweli na mengine uvumi tu.