Vampire? Jamaa aliyekamatwa akiri kuteka nyara, kunyonya damu na kuua kinyama watoto 10

Muuaji huyo alisema kuwa alikuwa akifurahia sana kutekeleza mauaji hayo.

Muhtasari

•Wanjala alikiri kuwa alikuwa na umri wa miaka 16 wakati aliua mhasiriwa wake wa kwanza, Purity Maweu ambaye alikuwa na miaka 12 tu alipokumbana na kifo chake.

•Kulingana na maafisa wa DCI, Wanjala alitekeleza mauaji hayo bila huruma kwa wakati mwingine akinyonya damu kutoka kwa mishipa ya watoto hao kabla ya kuwaua.

Image: DCI

Jamaa aliyekamatwa Jumatano na kukiri kuteka nyara na kuua watoto wawili kinyama kisha kutupa miili yao maeneo ya Kabete amehusika kwenye mauaji zaidi ya kumi.

Wapelelezi wa DCI wamebaini kuwa Masten Milimu Wanjala, 20, ameua kinyama angalau watoto wengine kumi ndani ya kipindi cha miaka tano ambayo imepita.

Kulingana na maafisa wa DCI, Wanjala alitekeleza mauaji hayo bila huruma kwa wakati mwingine akinyonya damu kutoka kwa mishipa ya watoto hao kabla ya kuwaua.

Baada ya kutekeleza mauaji, Wanjala amekuwa akitupa mili ya wahasiriwa wake katika vichaka vilivyo maeneo ya Lower Kabete huku mili ingine ikitupwa kwenye mabomba ya maji taka maeneo mbalimbali jijini Nairobi na kuachwa kuozea hapo.

Wanjala alikiri kuwa alikuwa na umri wa miaka 16 wakati aliua mhasiriwa wake wa kwanza, Purity Maweu ambaye alikuwa na miaka 12 tu alipokumbana na kifo chake.

Maweu alikuwa ametekwa nyara maeneo ya Kiima Kimwe kaunti ya Machakos. Wanjala alinyonya damu ya msichana huyo na kumuacha aage.

Miaka mitatu baadae mnyama huyo aliua kinyama kijana wa miaka 13 maeneo ya Kimilili.Mauaji ya Aaron  ambacho kilisababisha maandamano makubwa katika kijiji cha Kamukunywa huku wanakijiji wakichoma nyumba iliyoaminika kuwa ya mshukiwa wa unyama huo.

Wanjala anadaiwa kuua wavulana wawili kutoka maeneo ya Kitengela na Mlolongo ambao alidanganya wakaingia kwa mtego wakekisha kuwaua na kutupa mili yao katika mabomba ya maji taka. Miili ya wawili hao bado haijapatikana.

Wapelelezi wamebaini kuwa  Wanjala alitumia sumu nyeupe ambayo alipulizia ama kulazimisha wahasiriwa wake kunywa kabla ya kuwaua.

Muuaji huyo ambaye hakuonekana kutishika alisema kuwa alikuwa akifurahia sana kutekeleza mauaji hayo.

Siku ya Jumatano Wanjala aliwaongoza wapelelezi hadi mahali alikuwa ametupa miili ya watoto wawili maeneo ya Kabete.