Mgutusho baada ya jamaa kukiri kubaka na kunyonga wasichana 5 wadogo Uasin Gishu

Evans Juma Wanjala amekiri kubaka wasichana watano wa kati ya umri wa miaka 10 na 15 kabla ya kuwanyonga hadi kufa kati ya mwezi Desemba 2019 na Juni mwaka huu.

Muhtasari

•Siku chache tu baada ya jamaa mmoja kukiri kuteka nyara, kunyonya damu na kuua kinyama angalau  watoto 10, mwingine amekamatwa na kukiri kuwa amebaka na kuua kinyama wasichana watano wadogo.

•Mnyama huyo alifichua orodha ya wahasiriwa wake watano; Linda Cherono (13), Mary  Elusa (14), Grace Njeri (12), Stacy Nabiso (10) na Lucy  Wanjiru (15) na kupeleka wapelelezi kwenye maeneo ambayo alitekelezea kila kitendo.

Image: TWITTER//DCI

Siku chache tu baada ya jamaa mmoja kukiri kuteka nyara, kunyonya damu na kuua kinyama angalau  watoto 10, mwingine amekamatwa na kukiri kuwa amebaka na kuua kinyama wasichana watano wadogo.

Evans Juma Wanjala amekiri kubaka wasichana watano wa kati ya umri wa miaka 10 na 15 kabla ya kuwanyonga hadi kufa kati ya mwezi Desemba 2019 na  Juni mwaka huu.

Inadaiwa kuwa mshukiwa huyo aliwadanganya wasichana kutoka maeneo mbalimbali kaunti ya Uasin Gishu  kuingia kwenye mtego wake kabla ya kuwapeleka mahali fiche kisha kuwabaka na kuwanyonga.

Mnyama huyo alifichua orodha ya wahasiriwa wake watano; Linda Cherono (13), Mary  Elusa (14), Grace Njeri (12), Stacy Nabiso (10) na Lucy  Wanjiru (15) na kupeleka wapelelezi kwenye maeneo ambayo alitekelezea kila kitendo.

Mwili wa mmoja wa wahasiriwa wa Wanaja, Linda Cherono ulipatikana  mnamo Juni 15  mwaka huu karibu na bwawa la Baharini ukiwa unaendea kuoza.

Mwili wa Cherono ulipatikana ukiwa nusu uchi ukiwa na ishara za kubakwa, kunyongwa na majeraha mengine. Wanjala anadaiwa kutumia mtindo huo huo kutekeleza mauji  hayo mengine manne.

Wanjala alifunga miili ya wahasiriwa wawili kwenye gunia akaifunika na mboga na kuiacha ioze.

Wapelelezi wamebaini kuwa jamaa huyo ni mhalifu wa kawaida na kuna vibali vya kukamatwa  vilivyotolewa dhidi yake.

Mwaka wa 2018 Wanjala alishtakiwa na tuhuma za kubaka wasichana wawili na akaachiliwa na dhamana baada ya kukanusha mashtaka. Baada ya kuachiliwa mshukiwa  alienda mafichoni.

Siku ya Jumanne jamaa mwingine wa miaka 20 kwa jina Masten Wanjala alikiri kuteka nyara, kunyonya damu na kuua watoto zaidi ya kumi.