Mazishi ya afisa Caroline Kangogo kupangwa baada ya upasuaji wa mwili kufanyika leo- Familia

Mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor anatarajiwa kuendeleza shughuli hiyo hivi leo baada ya kukosa kufanyika Ijumaa wiki iliyopita kama ilivyokuwa imepangiwa

Muhtasari

•Babake marehemu, Barnaba Kangogo alikuwa amelalamikia hatua ya  kuahirishwa kwa upasuaji wa mwili kubaini kilichosababisha kifo cha Caroline kwani walilazimishwa kuahirisha mazishi yake.

•Mark Kangogo ambaye ni nduguye marehemu amedai kuwa tarehe ya mazishi itapangwa baada ya upasuaji wa mwili kufanyika.

Image: HISANI

Habari na Mathews Ndanyi

Mwili wa afisa Caroline Kangogo anayedaiwa kujitoa uhai takriban siku 10 zilizopita umewasirishwa mjini Eldoret  asubuhi ya leo (Jumanne Julai 27) kutoka  chumba cha kuhifadhi maiti cha hopitali ya Iten County Referral ili kupatia nafasi shughuli ya upasuaji wa mwili kufanyika katika hospitali ya Moi Teaching  & Referral.

Mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor anatarajiwa kuendeleza shughuli hiyo hivi leo baada ya kukosa kufanyika Ijumaa wiki iliyopita kama ilivyokuwa imepangiwa.

Babake marehemu, Barnaba Kangogo alikuwa amelalamikia hatua ya  kuahirishwa kwa upasuaji wa mwili kubaini kilichosababisha kifo cha Caroline kwani walilazimishwa kuahirisha mazishi yake.

Mark Kangogo ambaye ni nduguye marehemu amedai kuwa tarehe ya mazishi itapangwa baada ya upasuaji wa mwili kufanyika.

Marehemu anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwa wazazi wake katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Daktari Oduor anatarajiwa kufika kutoka Nairobi ili kuendeleza shughuli hiyo.

Iliripotiwa kuwa Caroline alijitoa uhai kwa kujipiga risasi kichwani mnamo Julai 16, madai ambayo yaliibua mdahalo mkubwa baina ya Wakenya huku wengine wakitaka majibu kuhusiana na kifo chake.

Utata mkubwa ulizingira kifo cha afisa huyo huku baadhi ya Wakenya wakidai kuwa huenda aliuliwa kisha mpango ukachorwa kuwashawishi Wakenya kuwa alijitoa uhai mwenyewe.

Jumbe alizodaiwa kuacha kama ameandika zilienezwa mitandaoni na moja ya ombi lake lilikuwa azikwe nyumbani kwa wazazi wake.