Kenya yapokea msaada wa dozi 410,000 za chanjo ya AstraZeneca kutoka Uingereza

Chanjo hizo zinatarajiwa kusaidia katika juhudi za serikali kuhakikisha kuwa angalau Wakenya milioni 10 wataweza kuwa wamechanjwa kufikia Krismasi

Muhtasari

•Ndege iliyokuwa imebeba chanjo hizo ilitua katika uwanja wa ndege wa JKIA siku ya Jumamosi na kupokewa na maafisa kutoka wizara ya afya wakiongozwa na waziri Mutahi Kagwe.

•Siku ya Jumatano serikali ya Kenya ilitangaza kurejelewa kwa shughuli ya kupatia makundi muhimu  chanjo ya kwanza .

Image: TWITTER// WIZARA YA AFYA

Nchi ya Kenya imepokea msaada wa  dozi 410,000 za chanjo aina ya AstraZeneca kutoka Uingereza.

Ndege iliyokuwa imebeba chanjo hizo ilitua katika uwanja wa ndege wa JKIA siku ya Jumamosi na kupokewa na maafisa kutoka wizara ya afya wakiongozwa na  katibu wa utawala katika  wizara ya afya Mercy Mwangangi .

Chanjo hizo zinatarajiwa kusaidia katika juhudi za serikali kuhakikisha kuwa angalau Wakenya milioni 10 wataweza kuwa wamechanjwa kufikia Krismasi.

Katibu wa utawala katika wizara ya mambo ya Kigeni Ababu Namwamba ambaye alikuwepo pia kupokea dozi hizo alisema kuwa ushirikiano wa mataifa yote duniani utasaidia sana katika kupigana na janga la Corona.

"Ushirikiano wa mataifa duniani ni muhimu sana katika vita dhidi ya janga hili. Utahakikisha kuwa kuna usawa katika kupata chanjo za kuokoa maisha ya watu" Namwamba alisema.

Siku ya Jumatano serikali ya Kenya ilitangaza kurejelewa kwa shughuli ya kupatia makundi muhimu  chanjo ya kwanza .

Ili kuweza kuthibiti ugonjwa wa COVID-19, nchi inapaswa kuchanja angalau asilimia 60% ya wananchi wake.

Mwishoni mwa mwezi wa Mei, serikali ilikuwa imesitisha shughuli ya kupatiana chanjo ya kwanza kwa muda baada ya kushuhudia matatizo ya kupata dozi hizo.

Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa katika ziara yake Uingereza aliweza kupata dozi 817,000 za chanjo aina ya Oxford-AstraZeneca.