'Kama yeye ni gaidi, pia mimi ni gaidi' Sudi akashifu hatua ya serikali kumfurusha Harun Aydin nchini

Sudi amehimiza rais Kenyatta kukabiliana na naibu rais William Ruto moja kwa moja ila sio kupitia watu wasio na hatia.

Muhtasari

•Hakuna aliyeruhusiwa kumuona Aydin tangu kukamatwa kwake siku mbili zilizopita. Hata wakili wake hakuruhusiwa kumtembelea.

•Sudi alihimiza rais Kenyatta kukabiliana na naibu rais William Ruto moja kwa moja ila sio kupitia watu wasio na hatia.

•Wakili wa Aydin, Ahmed Nassir alisuta serikali kwa kile alisema ni matumizi mabaya ya idara za kisheria ili kujinufaisha.

Oscar Sudi na Ahmed Nassir wazungumza baada ya Harun Aydin kufukuzwa nchini Image: ANDREW KASUKU
Oscar Sudi na Ahmed Nassir wazungumza baada ya Harun Aydin kufukuzwa nchini Image: ANDREW KASUKU

Raia wa Uturuki ambaye alikamatwa Jumamosi baada ya kutua nchini kutoka Uganda amefurushwa nchini.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alifahamisha wanahabari  kuwa Harun Aydin alirejeshwa kwao kwa ufiche mapema asubuhi ya leo.(Julai 9)

Hakuna aliyeruhusiwa kumuona Aydin tangu kukamatwa kwake siku mbili zilizopita. Hata wakili wake hakuruhusiwa kumtembelea.

Mbunge Sudi alikashifu kitendo hicho na kusema kuwa serikali ya Kenya haikuwa na sababu tosha za kumfukuza raia huyo wa Uturuki.

"Serikali haikuwa na sababu  za kumfungulia mashtaka na ndio sababu wakamfukuza. Kama yeye ni gaidi basi pia mimi ni gaidi" Sudi alisema.

Sudi aliendelea kusisitiza kuwa bw Aydin ni mwekezaji bali sio gaidi kama inavyodaiwa.

"Hawawezi kufuata katiba ambayo tuko nayo tayari na eti wanataka katiba mpya" Sudi aliendelea kukashifu hatua ya kufukuzwa kwa Aydin.

Wakili wa Aydin, Ahmed Nassir alisuta serikali kwa kile alisema ni matumizi mabaya ya idara za kisheria ili kujinufaisha.

"Kufukuza mtu nchini hufanyika kisheria . Tutapinga hatua ya serikali na tutamrejesha tena Bw Aydin" Nassir alisema.

Alisema kuwa hatua hiyo ni ya kisiasa na ni sharti wataipinga.