2 wauawa katika vurumai mtaani Kahawa West, Nairobi

Muhtasari

• Watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi Jumatano asubuhi wakati kundi moja wakaazi wa Kahawa West mjini Nairobi, walipoandamana kupinga ubomoaji wa mali zao.

Angalau watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi Jumatano asubuhi wakati kundi moja wakaazi wa Kahawa West mjini Nairobi, walipoandamana kupinga ubomoaji wa mali zao.

Wakazi ambao walimiliki mijengo kando ya barabara inayoelekea kwenye gereza la Kamiti kutoka eneo la Farmers Choice waliamka na kupata majengo yao yamebomolewa na mamlaka.

Eneo hilo kwa kawaida huwa na misongamano ya watu wanaotembea kwa miguu na magari.

Ubomoaji huu uliwafanya waandamane, wakidai kutofahamishwa na kupoteza mali ya thamani ya mamilioni ya pesa.

Polisi walisema waandamanaji hao walikuwa wamefunga barabara, na kusambaratisha  shughuli za kawaida huku wengine wakitumia hali hiyo kupora, na kulazimisha polisi kutumia risasi.

Mafunzo katika taasisi za elimu katika eneo hilo yaliathirika kwa muda mfupi wakati wa maandamano hayo.

Polisi walitumia nguvu, pamoja na risasi na gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji ambao walikuwa wamezua fujo na uporaji.

Baadhi ya waandamanaji walibeba mwili wa mwathiriwa, wakizuia polisi kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti.

Kulingana na polisi, baadhi ya vibanda viliporwa huku baadhi ya waandamanaji wakiwa walevi.

Mali ya thamani isiyojulikana iliharibiwa wakati mamlaka ilibomoa nyumba kutoa nafasi kwa upanuzi wa barabara.

“Hakuna ilani iliyotolewa kwetu kuhusu ubomoaji huu. Tumepoteza mali ambayo ilikuwa chanzo chetu cha kuishi, ”alisema mmoja wa watu walioathirika.

Maafisa zaidi wa usalama walipelekwa kutuliza hali hiyo.

Mkuu wa polisi wa Kiambu Ali Nuno alisema walilazimika kuingilia kati ili kurejesha hali ya utulivu.

Alisema mamlaka zinazohusika zitachunguza tukio hilo.