Makamishna wateule wa IEBC waapa kutojiuzulu licha ya shinikizo

Muhtasari

• Wajumbe wa kamati ya sheria ya bunge walikuwa wametafuta hakikisho kwamba wanne hao hawatatoroka nchini bila onyo lolote, haswa wakati wa uchaguzi.

Kamishna Mteule wa IEBC Juliana Cherera Picha: EZEKIEL AMING'A
Kamishna Mteule wa IEBC Juliana Cherera Picha: EZEKIEL AMING'A

Wateule wanne kwa nyadhifa za makamishna wa tume ya IEBC wamehakikishia Bunge kwamba watasalia ofisini hata wakati mambo yatachacha katika tume hiyo.

Wanne hao walisema hawatakubali shinikizo za ndani na nje na kuwafanya wajiuzulu, na kuwacha nchi katika hali ya swintofahamu.

Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Abonyo siku ya Jumanne waliahidi Kamati ya Haki na Sheria ya Bunge kuwa watasalia katika tume hiyo hata wakati mgumu.

Wajumbe wa kamati hiyo walikuwa wametafuta hakikisho kwamba wanne hao hawatatoroka nchini bila onyo lolote, haswa wakati wa uchaguzi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Muturi Kigano alielezea kumbukumbu za baadhi ya makamishna walioacha kazi katika kipindi cha uchaguzi uliopita na karibu watumbukize nchi katika mgogoro wa kisiasa.

Alisema kamati hiyo haitataka kamishna ambaye siku moja ataamka na kujiuzulu bila kuzingatia athari za uamuzi wake.

"Hatutaki watu ambao watatupa nchi kwa urahisi katika mgogoro wa kikatiba."

"Tunataka kujua ikiwa utabaki ofisini hata wakati kuna shinikizo kutoka kwa umma au hata wanasiasa kuacha kazi, haswa wakati wa uchaguzi.” Kigano alisema wakati Cherera alikuwa akitoa maoni yake.

Cherera alisema hatajiuzulu kwa sababu ya shinikizo, haswa kutoka kwa wanasiasa.

"Ikiwa mambo yatakuwa mabaya, nitabaki mahali hapo. Nitakuwa kama nahodha. Unajua nahodha hataacha meli," akaongeza.

Cherera alisema kila wakati ataweka masilahi ya umma mbele. "Nitazungumzia wanyonge na wale ambao hawana sauti," alisema.

Wanderi alisema kuondoka kwa tume kabla tu au baada ya uchaguzi ni kukosa uzalendo.

Mnamo Aprili 2018, tume ya IEBC ilipata pigo kubwa baada ya makamishna watatu kujiuzulu mara moja.

Consolata Maina, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya walisema wamepoteza imani na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati, na kusababisha kujiuzulu kwao.

Wanne hao walijiuzulu miezi sita baada ya kamishna Roselyne Akombe kujiuzulu, akitoa mfano wa IEBC kutoweza kufanya uchaguzi wa kuaminika kwa sababu ya kuingiliwa kisiasa.

Akombe alijiuzulu siku chache kabla ya uchaguzi wa marudio wa urais wa Oktoba 26 na kutoroka nchini.