Ruto na Uhuru wanyanyuana hadharani

Naibu wa rais amesema kwamba hatotishika na vitisho kutoka kwa maafisa wa serikali aliodai wanafadhaisha kampeni zake

Muhtasari

• Ruto ameapa kusalia katika utawala wa chama cha Jubilee na kwamba hatosalimu amri.

• Naibu wa rais amesema kwamba hatotishika na vitisho kutoka kwa maafisa wa serikali aliodai wanafadhaisha kampeni zake

Naibu rais William Ruto
DP Ruto Naibu rais William Ruto
Image: Twitter

Naibu wa rais William Ruto siku ya Jumanne alisema kwamba hatojiuzulu saa chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwataka wale wasioridhika na serikali yake kuondoka.

Ruto ameapa kusalia katika utawala wa chama cha Jubilee na kwamba hatosalimu amri licha ya wito wa kumtaka ajiuzulu iwapo hakubaliani na ajenda ya rais Uhuru Kenyatta kuliunganisha taifa.

Naibu wa rais amesema kwamba hatotishika na vitisho kutoka kwa maafisa wa serikali aliodai wanafadhaisha kampeni zake kukuza ajenda yake ya uchumi wa Chini kupanda juu {Bottom Up} nchini.

‘’Mimi ni mtu mwenye maono na sina nafasi ya kusalimu amri’’, alisema Dkt William Ruto huko huko Kinango Kwale. Naibu huyo alikuwa akizungumzakatika eneo bunge la kinango kaunti ya Kwale..

Wakati huohuo naibu huyo wa rais alipigia chapuo ajenda yake ya uchumi wa kuimarisha hali ya watu wa chini akisema kwamba alianzisha mazungumzo ambayo Wakenya wengi wamekuwa wakiyakubali.

Alisema kwamba mfumo huo wa uchumi utahakikisha kwamba watu wasio na ajira , wafanyabiashara wadogo wadogo wanaojaribu kujikimu kimaisha wanashirikishwa katika taifa.

Wakati huohuo naibu huyo wa rais amewaambia washindani wake kwamba Kenya sio taifa la watu wachache tu .

‘’Wanafaa kuelewa kwamba mimi ni mtu ambaye siwezi kusalimu amri na nimeamua kubadilisha uchumi kupitia vuguvugu la Hustler na mfumo wa kiuchumi wa ‘Bottom up’.

Aliwashutumu waliowa wakiunga mkono muswada wa BBI kwa kuwa na maslahi ya kibinafsi na ajenda bila kuwajali Wakenya masikini.

‘’Tunataka kujenga taifa ambalo hakuna hata Mkenya mmoja atawachwa nyuma.

Hatutakubali watu wachache kuendeleza maslahi yao ya kibinafsi kwa kubadilisha katiba ili kugawanya nyadhfa bila kuwajali mamilioni ya Wakenya ambao hawana ajira’’, alisema.

Akizungumza na wahariri siku ya Jumatatu , rais Uhuru Kenyatta hakuficha kukasirishwa kwake na ukosoaji uliotolewa dhidi ya utawala wake na kambi ya Ruto .

Rais alisema hakuwa na ufahamu wowote kwa nini upande wa DP Ruto umechagua mashambulio dhidi ya utawala wake .

Aliwaambia waandishi wa habari jijini Nairobi kwamba hakuwa na shida na Ruto kujenga ngome yake kisiasa lakini alihoji njia ambazo timu ya UDA inatumia. UDA ni chama kipya kinachoungwa mkono na naibu wa rais.