6 wafariki katika ajali ya barabarani - Nakuru

Muhtasari

• Kamanda wa polisi wa Nakuru, Beatrice Kiraguri alisema waliofariki walikuwa wanaume watano na mwanamke mmoja.

• Kiraguri alisema dereva wa lori alishindwa kulidhibiti, na kugongana na matatu.

Image: NYAKERU KARIRE

Watu sita walifariki Jumatano jana karibu na shule ya Shiners Boys kwenye barabara kuu ya Nakuru wakati lori lilipogongana ana kwa ana na gari la abiria.

Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Nakuru, Beatrice Kiraguri alisema waliofariki walikuwa wanaume watano na mwanamke mmoja.

Alisema dereva wa abiria la kampuni ya North Rift Shuttle ni miongoni mwa wale ambao waliaga.

"Haijulikani ni watu wangapi walinusurika kutokana na ajali hiyo lakini maafisa wa polisi watazuru hospitali kuhakikisha idadi kamili," alisema.

Kiraguri alisema kulingana na muongozo na taratibu za kampuni ya uchukuzi ya North Rift, matatu ilikuwa na abiria saba.

Image: NYAKERU KARIRE

"Hatuwezi kusema kwa hakika kuwa ilikuwa na abiria saba kwa sababu mtu hawezi kuwa na hakika ikiwa dereva alichukua wasafiri wa ziada njiani," alisema.

Kiraguri alisema dereva wa lori alishindwa kulidhibiti, na kugongana na matatu.

Aliongeza kuwa idadi ya watu waliokuwa ndani ya lori wakati wa ajali hiyo ya saa kumi na mbili unusu haijulikani pia.

"Lori lilikuwa likielekea Nairobi na matatu ilikuwa ikienda upande mwingine," alisema.

Kamanda huyo alisema miili ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Kaunti ya Nakuru huku mabaki ya magari yakipelekwa kwa Kituo cha Polisi cha Nakuru.