Ruto anafaa kujiuzulu, Raila amuunga Uhuru mkono

Alirejelea wakati alijiuzulu kama mbunge wa Lang’ata kujitenga na chama ambacho kilikuwa kimehusishwa na kashfa ya Goldenberg.

Muhtasari

• Ukiona mambo si sawa na wewe ni mtu mwenye msimamo, sema tu mambo sio sawa na ujiuzulu," Raila alisema.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga ameunga mkono ombi la Rais Uhuru Kenyatta kuwa Naibu rais William Ruto anafaa kujiuzulu ikiwa haridhishwi na serikali ya sasa.

Waziri Mkuu wa zamani alisema litakuwa jambo la heshima kwa mwanasiasa yeyote kufanya, akitoa wito kwa wabunge wa Jubilee ambao wamehamia UDA pia kufuata mkondo na kujiuzulu ili wagombeE nyadhifa zao kwa chama chao kipya UDA.

"Ukiona mambo si sawa na wewe ni mtu mwenye msimamo, sema tu mambo sio sawa na ujiuzulu," Raila alisema, akitoa mfano wa unafiki.

"Wabunge hawa wakisema wako katika UDA na bado wanapata mshahara kupitia Jubilee pia wanapaswa kujiuzulu, warudi kwa watu na kutetea viti na chama kipya."

"Huo unaitwa msimamo thabiti wa kisiasa, mengineo ni unafiki," Raila alisema, na kuongeza kuwa haikuwa mara ya kwanza Kenya kuwa na Makamu wa Rais.

“Baba yangu alikuwa makamu wa rais wa kwanza. Hakungoja kufutwa kazi. Alipoona kuwa mambo yamebadilika na ametengwa, aliandika barua. ”

Raila alinukuu barua ya baba yake iliyosema, "Siwezi kuhalalisha kupata mshahara wa umma bila uwajibikaji. Kizazi kijacho kitaniangalia bila huruma na kwa sababu hii, najiuzulu wadhifa huu. ”

Alirejelea wakati alijiuzulu kama mbunge wa Lang’ata kujitenga na chama ambacho kilikuwa kimehusishwa na kashfa ya Goldenberg.

"Wakati nilikuwa mbunge wa Langata chini ya Ford Kenya, tuliona Goldenberg ... nikasema siwezi kuendelea kuwa mbunge chini ya Ford Kenya na nikajiuzulu."

"Nilisema nitarudi na chama kingine ... na nikagombea kiti changu kwa tikiti ya NDP na nikachaguliwa tena."