COVID 19: Wagonjwa 6935 wanaendelea kupokea matibabu; 1280 wapata nafuu

Asilimia ya maambukizi kwa sasa imesimamia 12.6%.

Muhtasari

•Kenya imeripoti  visa vipya 565 vya wagonjwa wa COVID-19 kutoka kwa sampuli ya watu 4,494 ambao wameweza kupimwa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

•Vifo 6 zaidi vimeripotiwa na kufikisha idadi ya walioangamia nchini kutokana na maradhi ya COVID-19 kuwa 4726

Waziri Mutahi Kagwe
Waziri Mutahi Kagwe
Image: MOH

Wizara ya afya leo hii imetangaza visa vipya 565 vya wagonjwa wa COVID-19 kutoka kwa sampuli ya watu 4,494 ambao wameweza kupimwa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Idadi  hii imefikisha jumla ya visa vilivyowahi kuripotiwa nchini kuwa 235,863 kutoka kwa vipimo 2,371,571 ambavyo vimefanywa tangu kuingia kwa virusi vya Corona nchini.

Asilimia ya maambukizi  kwa sasa imesimamia 12.6%.

Kaunti ya Nairobi ilirekodi visa 157 ikifuatiwa na Kiambu iliyoripoti visa 95. Kaunti ya Nakuru iliandikisha visa 73 huku kaunti zingine zikiandikisha visa chini ya 50 kila mmoja.

Mtoto wa miezi 11 na mkongwe wa miaka 95 ni miongoni mwa waliopatikana na virusi hivyo siku ya leo.

Wagonjwa 1280 wameweza kupata nafuu, 1062 wakipona kutoka manyumbani huku wengine 218 wakipewa ruhusa kutoka vito mbalimbali vya afya nchini.

Wagonjwa 1898 wanaendelea kupokea matibabu katika vituo mbalimbali vya afya nchini huku wengine 5,037 wakiendelea kujitenga nyumbani. Wagonjwa 160 wamelazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi.

Vifo 6 zaidi vimeripotiwa na kufikisha idadi ya walioangamia nchini kutokana na maradhi ya COVID-19 kuwa 4726.

Chanjo ya Corona

Kufikia sasa watu 1,968,656 wameweza kupokea angalau dozi moja ya chanjo dhidi ya Corona huku watu 804,583 wakiwa wamepokea dozi zote mbili.