Rais Uhuru Kenyatta atuma risala za rambirambi kwa familia ya Dedan Kimathi

Muhtasari
  • Rais Uhuru Kenyatta atuma risala za rambirambi kwa familia ya Dedan Kimathi
Peris Muthoni
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa pole kwa Mama Mukami Kimathi na familia nzima ya shujaa wa uhuru wa Kenya Dedan Kimathi kufuatia kifo cha binti yao Peris Muthoni Kimathi.

Marehemu Muthoni Kimathi alifariki mwishoni mwa wiki baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Katika ujumbe wake wa faraja, Rais alimtaja marehemu Muthoni kama mtu mchangamfu na nguzo madhubuti ya familia ya mpigania uhuru aliyemtunza sana Mama Mukami Kimathi.

"Ni bahati mbaya kwamba tumempoteza Muthoni Kimathi kwa mkono mbaya wa kifo wakati familia yake, haswa Mama Mukami Kimathi, ilimuhitaji zaidi kama mlezi wa karibu," Rais alisema.

Rais alimkumbuka Muthoni kama mtu mchangamfu ambaye alijitahidi kuhakikisha Mama Mukami Kimathi, mjane mzee wa mpigania uhuru Dedan Kimathi, anatunzwa vizuri na kuwaombea faraja ya Mungu wakati wanakabiliana na wakati huu mgumu.

"Muthoni alikuwa kando ya Mama Mukami Kimathi, akimtunza na kuhakikisha anahudumiwa vizuri. Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia ya Dedan Kimathi, haswa kwa Mama Mukami, na ninaomba kwamba Mungu awape faraja katika kipindi hiki kigumu, "Rais aliomboleza.