Serikali yashtakiwa kwa kuhamisha maafisa wa GSU waliokuwa wanalinda naibu rais Ruto

Walalamishi hao wanataka mahakama itoe amri ya kurejeshwa kwa maafisa hao mara moja.

Muhtasari

•Walalamishi wamesema kuwa hatua hiyo itadhoofisha kazi ambayo naibu rais anafaa kufanyia Wakenya kulingana na katiba.

Naibu Rais akikaribisha maafisa wa AP kwake Karen
Naibu Rais akikaribisha maafisa wa AP kwake Karen
Image: DPPS

Wakenya wawili wamefika mahakamani kushtaki serikali kwa kuhamisha maafisa wa GSU waliokuwa wanalinda makazi ya naibu rais William Ruto wiki iliyopita.

Miruru Waweru na Angela Mwikali wamedai kuwa hatua ya kuondolewa kwa maafisa hao na sio ya kisheria na kuwa inakiuka katiba ya Kenya.

Wamesema kuwa hatua hiyo itadhoofisha kazi ambayo naibu rais anafaa kufanyia Wakenya kulingana na katiba.

Walalamishi wawili hao wanataka mahakama itoe amri ya kurejeshwa kwa maafisa hao mara moja.

Siku ya Alhamisi wiki iliyopita maafisa wa GSU waliokuwa wanalinda makazi rasmi ya Ruto  maeneo ya Karen walihamishwa na nafasi hiyo kuchukuliwa na polisi wa AP.