Ulinzi wa Ruto: Naibu rais ana walinzi 257 - Matiang'i

Muhtasari

• Kulinga na Matiangi naibu rais analindwa na jumla ya maafisa 257 wa polisi.

• Waziri Matiang’i aliwakikishia wakenya kuhusu usalama wa naibu rais.

• Ruto ana Makomando 74 wa kikosi maalum cha ulinzi wa rais, maafisa 5 wa GSU, na maafisa sita kutoka idara ya DCI, hawa wote ni wa usalama wa karibu wa naibu rais.

Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i na katibu wa kudumu wa usalama Karanja Kibicho walipofika mbele ya kamati ya bunge ya usalama kujibu maswali kuhusu usalama wa naibu rais William Ruto mnamo 1/9/2021.
Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i na katibu wa kudumu wa usalama Karanja Kibicho walipofika mbele ya kamati ya bunge ya usalama kujibu maswali kuhusu usalama wa naibu rais William Ruto mnamo 1/9/2021.

Naibu rais William Ruto ndiye kiongozi katika wadhifa wowote chini ya rais nchini Kenya kuwahi kulindwa na idadi kubwa zaidi ya maafisa wa usalama katika historia ya Kenya.

Kulinga na stakabdhi zilizowasilishwa katika kamati ya bunge ya ulinzi na waziri wa Usalama Fred Matiangi siku ya Jumatano naibu rais analindwa na jumla ya maafisa 257 wa polisi.

"Hatujadunisha usalama wa naibu huyo. Mabadiliko mapya walifanywa na Inspekta mkuu wa polisi. Utaratibu huo ulikuwa sawa ," Matiang'i alisema.

Waziri Matiang’i alisema kwamba usalama wa naibu rais unatekelezwa kwa awamu tatu: 

  1. Makomando 74 wa kikosi maalum cha ulinzi wa rais, maafisa 5 wa GSU, na maafisa sita kutoka idara ya DCI, hawa wote ni wa usalama wa karibu wa naibu rais.
  2. Maafisa 121 kutoka vitengo vya APS, SGB na CIPU.
  3. Maafisa wa ziada 51 wanaotoa ulinzi kwa majengo mbali mbali yanayomilikiwa na naibu.

Waziri Matiang’i aliwakikishia wakenya kuhusu usalama wa naibu rais.

“Hakuna cha kuhofia kuhusu usalama wa naibu rais, tuko na maafisa wa kutosha wenye tajiriba ya juu kumpa naibu rais ulinzi,” Matiang’i alisema.

Matiang’i alihoji mjadala uliyoibuliwa kutokana na uhamisho uliofanywa katika ulinzi wa makazi ya naibu rais akisema kwamba huenda ulichochewa mazingira ya kisiasa nchini kwa sasa. Alisema serikali itutaendelea kutoa huduma za usalama kwa naibu rais kwa njia mwafaka na kuambatana na muongozo wa sheria.

Kulingana na Matiang’i jumla ya maafisa wa usalama 51 wa ziada wanatumika kutoa ulinzi kwa mali mbali mbali za naibu rais kutoka nchini kama ifuatavyo.

Wanasiasa wanaogemea mrengo wa Tanga tanga waliibua mjadala kuhusu usalama wa naibu rais baada ya kudai kwamba usalama wake ulikuwa umedunishwa kufuatia hatua ya idara ya polisi kuondoa maafisa wa GSU waliokuwa wakilinda makazi rasmi ya Ruto mtaani Karen na kuleta maafisa wa AP. 

Matiang'i akiwa mbele ya kamati ya Bunge pia alisema kwamba taratibu za kuadhibu maafisa wa serikali zitatumika dhidi ya afisa mkuu wa wafanyikazi katika ofisi ya naibu rais aliyemkosoa kwa kuweka kwa mtandao wa kijamii barua rasmi aliyokuwa amemuandikia Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai kuhusu mabadiliko katika ulinzi wa naibu rais.