Mshukiwa wa Al Shabaab auawa Mandera bunduki 5 zapatikana

Muhtasari

• Mbali na bunduki tano za AK47, polisi walisema pia walipata zaidi ya risasi 500.

• Hakuna afisa wa polisi aliyejeruhiwa katika kisa hicho kilichotokea karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Silaha zilizopatikana kutoka kwa washukiwa wa ugaidi wa al-shabaab mnamo Septemba 2 huko Mandera Picha: NPS
Silaha zilizopatikana kutoka kwa washukiwa wa ugaidi wa al-shabaab mnamo Septemba 2 huko Mandera Picha: NPS

Jamaa aliyekuwa amejihami kwa bunduki anayeaminika kuwa mshiriki wa al Shabaab aliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa makabiliano na polisi katika eneo la Kutulo, kaunti ya Mandera, na bunduki tano kupatikana kutoka kwake.

Tukio hilo lilitokea Alhamisi alasiri wakati kikosi cha maafisa wa operesheni maalum walipopata watu wenye silaha katika eneo la Kutaiyo.

Polisi walisema maafisa wa kikosi hicho maalum walikuwa wakifanya doria katika eneo hilo walipokutana na watu wanne wenye silaha ambao walikuwa wamepanda pikipiki.

Walikabiliana vikali na kusababisha mauaji ya mmoja wa washukiwa huku wengine wakifanikiwa kutorokea kwenye pikipiki.

Mbali na bunduki tano za AK47, polisi walisema pia walipata zaidi ya risasi 500.

Hakuna afisa wa polisi aliyejeruhiwa katika kisa hicho kilichotokea karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Msako kuwatafuta washukiwa wengine haukuzaa matunda.

Kamanda wa polisi kanda ya kaskazini mashariki Rono Bunei alisema maafisa wameimarisha doria katika eneo hilo kukabili mashambulio ya hapa na pale kutoka kwa wanamgambo wa al Shabaab na wale wanaowaunga mkono.

Alihimiza ushirikiano kutoka kwa wakaazi katika juhudi za kukabiliana na ukosefu wa usalama, ambao umeathiri usafiri, elimu na maendeleo kwa jumla.

“Lazima tushirikiane kuhakikisha tunapunguza shughuli hizi ambazo zinakwamisha maendeleo. Ni jukumu la kila mtu kuhakikisha kuna usalama, ”Bunei alisema.

Eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto za usalama katika miezi iliyopita kutokana na mashambulio ya wanamgambo wa al Shabaab wanaovuka kutoka mpaka wa Somalia.

Maeneo hayo, ambayo ni pamoja na Mandera, Wajir, Garissa na Lamu yako karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, ambayo inafanya iwe rahisi kwa wanamgambo kushambulia kwa mapenzi yao.