Polisi 3 miongoni mwa waliouawa Laikipia

Muhtasari

• Kati ya hao wanane, watatu ni maafisa wa polisi waliokuwa wakishiriki katika kuwakabili wavamizi, huku watano ni raia.

• Raia ambao wamejeruhiwa na risasi ni wanne wakati maafisa wa polisi waliojeruhiwa ni wawili.

Mratibu wa Bonde la Ufa George Natembeya. Picha: JOSEPH KANGOGO
Mratibu wa Bonde la Ufa George Natembeya. Picha: JOSEPH KANGOGO

Watu wanane wameuawa kutokana na mapigano ya Laikipia katika kipindi cha mwezi mmoja uliyopita, Mratibu wa kanda ya Bonde la Ufa George Natembeya amesema.

Kati ya hao wanane, watatu ni maafisa wa polisi waliokuwa wakishiriki katika kuwakabili wavamizi, huku watano ni raia.

Akizungumza siku ya Jumatano, Natembeya alisema vifo hivyo vilitokea kabla ya shughuli ya usalama kuanza siku ya Jumanne.

"Raia ambao wamejeruhiwa na risasi ni wanne wakati maafisa wa polisi waliojeruhiwa ni wawili," alisema.

Natembeya alibainisha kuwa hakuna mashambulio yoyote yaliyotokea tangu operesheni ya usalama ya pamoja ianze.

“Hakuna tukio la uchomaji moto, majeruhi, kufurushwa au vifo ambalo limeripotiwa. Tumetoa usalama pia kwa wale wanaoondoka katika eneo hili ili wasinyanyaswe, ”alisema.

Natembeya aliwaonya wanasiasa kuachana na Laikipia akisisitiza kuwa huu sio wakati wao kufanya siasa.

Alishutumu viongozi wa eneo hilo kwa kufadhili vijana wanaosababisha machafuko katika eneo hilo kwa kuwapa chakula na bunduki, wakati wanaendeleza uvamizi wao.

"Tumepokea ripoti kwamba baadhi ya wamiliki wa mifugo wanasema wanaziondoa kwenye ranchi na wanaleta Morani 500 kupigana na maafisa wa usalama. Hii inamaanisha kuwa kuna mipango mahsusi ya mashambulizi ili kuhakikisha eneo hilo halina amani," Natembeya alisema.

Msemaji wa Polisi wa Bruno Shioso alisema operesheni ya usalama imesababisha kutolewa kwa wafugaji haramu kutoka Laikipia Nature Conservancy.

Pia alikanusha ripoti za shambulio la kuteketeza Shule ya Msingi Merigwiti kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari, akisema kwamba suala hilo linachunguzwa.