Watengezaji bidhaa Kenya watakiwa kuongeza thamani

Muhtasari

• 37%  ya biashara zinazoendeshwa chini ya mfumo wa EPZ zinamilikiwa na Wakenya ikilinganishwa na asilimia 40 inayomilikiwa na wawekazaji wa kigeni.

Waziri wa viwanda Betty Maina
Waziri wa viwanda Betty Maina
Image: Kwa HISANI

Watengenezaji bidhaa wa humu nchini wametakiwa kuongezea thamani bidhaa ili kufanikisha juhudi za serikali za kuafikia nguzo Nne za ajenda kuu ya maendeleo ikiwemo kilimo na uzalishaji.

Akizungumza huko Athi River Kaunti ya Machakos alipozuru eneo la kutengeneza bidhaa hizo EPZA siku ya Alhamisi Waziri wa Viwanda Betty Maina alivitaka viwanda vya humu nchini kutumia malighafi ya humu nchini kuwasaidia wakulima nyanjani.

Na ili kupunguza kiwango cha kutegemea malighafi kutoka nje na kuiwezesha Kenya kuuza bidhaa zake katika nchi za kigeni, Waziri alisema serikali inashauriana na Marekani kuona jinsi watengenezaji bidhaa chini ya mfumo wa EPZA watanufaika na soko hilo baada ya kukamilika kwa mpango wa AGOA.

Hata hivyo, Waziri alisema nchi ya Uingereza na Uropa tayari zimedhihirika kuwa soko muhimu la kigeni kwa bidhaa za humu nchini lenye masharti nafuu na ushindani wa kustahimili.

Akitoa hakikisho hilo, Waziri alisema serikali inatambua wamiliki wa viwanda chini ya mfumo wa EPZA wanaoendeleza uzalishaji kwa kutumia malighafi za humu nchini hatua aliyosema inawapa vijana nafasi za kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha MAS Kenya Milinda Jayasundura alisema mbali na kutoa nafasi za kazi kwa vijana nchini wanashirikiana kwa karibu na wauzaji bidhaa ndogo ndogo nchini ili kukidhi mahitaji ya soko la kigeni.

Katika kiwanda cha Africa Coffee Rosters, Waziri Maina aliarifiwa kwamba kahawa inayozalishwa humu nchini inaendelea kuwa bora zaidi katika masoko ya nje kufuatia matumizi bora ya teknolojia ya kisasa pamoja na utafiti.

Kwa upande wake, Balozi wa heri njema wa kampuni ya Coop Danmark inayoongoza kwa uuzaji wa bidhaa Sorcn Sylvest alisema wajibu wao ni kuhakikisha wakulima wa kahawa hapa nchini wananufaika na zao hilo kwa kunawiri katika soko la kigeni.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi wa EPZA Benjamin Chesang aliyesema kufikia sasa jumla ya uwekezaji wa biashara na maeneo ni shilingi bilioni 116.3 na kwamba halmashauri hiyo itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji.

Alisema asilimia 37 ya biashara zinazoendeshwa chini ya mfumo wa EPZ zinamilikiwa na Wakenya ikilinganishwa na asilimia 40 inayomilikiwa na wawekazaji wa kigeni na asilimia nyingine 22 inayomilikiwa kwa ushirikiano.