Mahakama yamzuia mkurugenzi wa NMS, Badi kuhudhuria mikutano ya mawaziri

Muhtasari

• Jaji Anthony Mrima alisema kwamba agizo la rais Nambari 3 la mwaka 2020 ni kinyume cha sheria.

• Badi alipewa jukumu la kubadilisha jiji la Nairobi na kukabili msururu wa ufisadi na utendakazi duni katika kaunti ya Nairobi.

Mkurugenzi mkuu wa Huduma za Metropolitan Nairobi Mohammed Badi. Picha: MAKTABA
Mkurugenzi mkuu wa Huduma za Metropolitan Nairobi Mohammed Badi. Picha: MAKTABA

Mahakama kuu ya Milimani imefutilia mbali uamuzi wa Rais Uhuru Kenyatta uliomteua na kumjumuisha Luteni Jenerali Mohamed Badi katika mikutano ya Baraza la Mawaziri.

Jaji Anthony Mrima alisema kwamba agizo la rais Nambari 3 la mwaka 2020 ni kinyume cha sheria.

Alitoa pia amri ya kuzuia Badi kuhudhuria mikutano yoyote ya Baraza la Mawaziri au kutekeleza majukumu yoyote ya Baraza la Mawaziri.

“Hakuna shaka uteuzi wa Badi katika Baraza la Mawaziri haukuidhinishwa na Bunge. Kwa hivyo haijulikani ni nani na nani Badi atapigwa msasa na kazi yake kuwekwa kwenye darubini. Majukumu yake ya uajiri katika Baraza la Mawaziri pia hayajulikani,”jaji alisema.

Mrima pia alisema hapati sababu yoyote muhimu kumjumuisha Badi katika Baraza la Mawaziri.

Katika kesi hiyo, Mbunge wa Kandara Alice Wahome alikwenda mahakamani kupinga uhalali wa kumteua na kumjumuisha Badi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa huduma za Metropolitan Nairobi katika Baraza la Mawaziri na kamati zake.

Badi alipewa jukumu la kubadilisha jiji la Nairobi na kukabili msururu wa ufisadi na utendakazi duni katika kaunti ya Nairobi.

NMS iliwekwa madarakani mnamo Machi 18, 2020, na Rais, karibu mwezi mmoja baadaye Gavana wa Nairobi Mike Sonko alikabidhi majukumu manne muhimu kwa serikali ya kitaifa.

Kazi zilizohamishwa ni huduma za afya za kaunti, uchukuzi, kazi za umma, huduma na huduma muhimu na mipango na maendeleo ya kaunti hiyo.