IPOA kuchunguza matukio mawili ambapo polisi wanadaiwa kupiga raia risasi jijini Nairobi na Nyeri

Muhtasari

•Jamaa mmoja aliangamia kutokana na jeraha la risasi ambayo alipigwa siku ya Jumamosi kwenye barabara ya Kirinyaga jijini Nairobi huku mwingine aliyepigwa risasi katika eneo bunge la Mathira usiku wa Ijumaa akiendelea kuhudumiwa hospitali akiwa katika hali mahututi.

Anne Makori mwneyekiti wa IPOA

IPOA imeanza uchunguzi kuhusiana na matukio mawili ambapo polisi wanadaiwa kupiga raia risasi katika kaunti Nyeri na jijini Nairobi.

Jamaa mmoja aliangamia kutokana na jeraha la risasi ambayo alipigwa siku ya Jumamosi kwenye barabara ya Kirinyaga jijini Nairobi huku mwingine aliyepigwa risasi katika eneo bunge la Mathira usiku wa Ijumaa akiendelea kuhudumiwa hospitali akiwa katika hali mahututi.

Mwenyekiti wa IPOA Bi Anne Makori amesema wanachunguza matukio hayo mawili na kutoa hakikisho kwamba watatoa mapendekezo ya hatua itakayochukuliwa iwapo yeyote atapatikana na hatia .

Siku ya Jumamosi waendesha  bodaboda jijini Nairobi walishiriki maandamano wakilalamikia matumizi mabaya ya nguvu za polisi baada ya mmoja wao kufariki kutokana na kile kinachodaiwa  kwamba alipigwa risasi na polisi.

Kulingana na waandamanaji hao ambao waliandamana katika barabara ya Kirinyaga, polisi mmoja anayefanya kazi katika kituo cha polisi cha Kamukunji alipiga mmoja wao risasi baada ya kukataa kutoa hongo. Hata hivyo, haijathibitishwa rasmi yaliyojiri kwenye tukio hilo.

Afisa mwingine wa polisi anadaiwa kupiga kijana mmoja risasi katika  eneo la Mathira, kaunti ya Nyeri mida ya saa moja usiku wa Ijumaa.

Kulingana na mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, polisi kutoka kituo cha Gatung'ang'a walimpiga kijana huyo risasi na kumuacha akiwa hali mahututi alipokuwa anajaribu kuwazuia wasiendelee kunyanyasa baba yake.

Kijana huyo alikimbizwa katika hositali ya Karatina ambako anaendelea kuhudumiwa.

Gachagua aliagiza kukamatwa kwa afisa aliyehusika kwenye tukio hilo na kuomba marekebisho kufanywa katika kituo cha polisi cha Gatung'ang'a.

Raia wameagizwa kuwa watulivu huku IPOA ikiendelea na uchunguzi wake.