"Wahubirieni" Naibu Rais William Ruto ahimiza viongozi wa dini wasifukuze wanasiasa kanisani

Muhtasari

•Ruto alisema kwamba neno la Mungu linaweza hubiriwa kwa njia nyingi na kudai kwamba amefanya bidii kubwa kuleta wanasiasa kanisani.

•Hata hivyo msaidizi huyo wa rais Kenyatta alisema kwamba anaunga mkono hatua ya viongozi wa dini kuzuia wanasiasa kutumia madhabahu kutusi wapinzani wao.

Naibu rais William Ruto
DP William Ruto Naibu rais William Ruto
Image: Maktaba

Naibu rais William Ruto ameomba viongozi wa dini kutozuia wanasiasa kanisani na badala yake wawahubirie.

Alipokuwa anahutubia waumini katika kanisa ya AIPCA Meru, Ruto alisema kwamba neno la Mungu linaweza hubiriwa kwa njia nyingi na kudai kwamba amefanya bidii kubwa kuleta wanasiasa kanisani.

"Nataka kuomba maaskofu na viongozi wengine wa kanisa wasifukuze hawa watu. Wahubirieni" Ruto alisema.

"Nimefanya kazi kubwa, baadhi ya wanasiasa hawa hawakuwa wanakuja kanisani lakini sasa wameanza kuja kwa sababu wananiona nikikuja. Mungu ameendelea kunisukuma na wanafahamu kwamba yeye ni kila kitu" Alisema.

Hata hivyo msaidizi huyo wa rais Kenyatta alisema kwamba anaunga mkono hatua ya viongozi wa dini kuzuia wanasiasa kutumia madhabahu kutusi wapinzani wao.

Alisihi wanasiasa wote kuheshimu kanisa kila wanapopatiwa nafasi ya kuzungumza.

"Tunahitaji kuwa na mipaka kama viongozi wa Kikristo. Tusileta ugomvi wetu wa kisiasa kwenye madhabahu" Ruto alsisema.

Matamshi ya Ruto yanakuja wiki mbili tu baada ya  makanisa kadhaa kupiga marufuku hotuba za wanasiasa kanisani.

(Utafsiri: Samuel Maina)