Afghanistan: Biden alishauriwa kubakisha wanajeshi 2,500

Muhtasari

• Taliban ilichukuwa madaraka mwezi Agosti baada ya wapiganaji wake kufanikiwa kupiga hatua hadi mjini Kabul na maeneo mengine ya nchi bila upinzani wowote.

Image: GETTY IMAGES

Majenerali wawili wakuu wa jeshi nchini Marekani wamesema kwamba walipendekeza kubakia kwa wanajeshi 2500 nchini Afghanistan , kabla ya Marekani kuwaondoa wanajeshi wote mwezi Agosti.

Ushuhuda wa jenerali Mark Milley na Jenerali Frank McKenzie katika bunge la Congress ulionekana kukinzana na tamko la rais Joe Biden aliyesema kwamba hakumbuki kupata ushauri kama huo.

Taliban ilichukuwa madaraka mwezi Agosti baada ya wapiganaji wake kufanikiwa kupiga hatua hadi mjini Kabul na maeneo mengine ya nchi bila upinzani wowote.

Jenerali Milley alisema kwamba Marekani ilishangazwa na kasi ya kuanguka kwa serikali ya Afghanistan. Majenerali hao wawili waliulizwa na kamati ya bunge la seneti kuhusu huduma za jeshi pamoja na waziri wa ulinzi Lloyd Austin siku ya Jumanne.

 

kikao hicho kinajiri wiki kadhaa baada ya kuondoka kwa ghafla kulikoshuhudiwa katika uwanja wa ndege wa kabul huku mataifa ya kigeni yakijaribu kuwaondosha raia wao huku nao maelfu ya raia wa taifa hilo wakiomba kuokolewa.

Shambulio la kujitolea muhanga liliwaua watu 182 wakati wa operesheni hiyo ya kuondoka .

Wanajeshi 13 wa Marekani na raia 169 wa Afghanistan waliuawa katika lango la uwanja wa ndege wa Kabul mnamo tarehe 26 mwezi Agosti.

Kubakisha wanajeshi nchini humo

Jenerali McKenzie , ambaye akiwa mkuu wa majeshi ya Marekani alisimamia kuondoka kwao , alisema chini ya masuali makali kutoka kwa maseneta wa chama cha Republican kwamba alipendekeza kubakishwa kwa kikosi kidogo cha wanajeshi 2,500 nchini Afghanistan.

Tamko lake lilionekana kukinzana na matamshi ya Joe Biden akizungumza na mwandishi wa ABC tarehe 19 Agosti kwamba hakumbuki mtu yeyote akimpatia ushauri kama huo.

Jenerali Milley alisema kwamba alikubaliana na mapendekezo hayo , lakini alipoulizwa na seneta wa Alaska Dan Sullivan iwapo matamshi ya Joe Biden yalikuwa ya uwongo, alikataa kutoa jibu la moja kwa moja.

Baadaye msemaji wa Whitehouse Jen Psaki alisema alizungumzia kuhusu suala hilo.

"Rais anathamini ushauri wa wakuu hao wa jeshi'' , alisema. Lakini hio haimaanishi kwamba anakubaliana nao. Alisema kwamba iwapo wanajeshi wagesalia nchini humo baada ya siku ya mwisho ya kuondoka mwezi Agosti , Marekani hivi sasa ingekuwa katika vita na Taliban.