Majambazi wavamia tena Laikipia na kuiba mifugo

Muhtasari

•Kulingana na ujumbe ambao ulitolewa na idara ya polisi nchini (NPS), genge la majambazi liliweza kupita maafisa wa usalama na vizuizi vilivyowekwa na kuiba mifugo katika kijiji cha Ndunyu, eneo la Kirima.

•Kikosi kinachohusisha maafisa wa polisi na wanajeshi wa KDF wameanza juhudi za kuwawinda washukiwa na kurejesha mifugo ambao waliibiwa.

crime scene 1
crime scene 1

Takriban wiki mbili tu baada ya hali ya utulivu kurejea katika kaunti ya Laikipia, majambazi wamevamia tena na kuiba mifugo.

Kulingana na ujumbe ambao ulitolewa na idara ya polisi nchini (NPS), genge la majambazi liliweza kupita maafisa wa usalama na vizuizi vilivyowekwa na kuiba mifugo katika kijiji cha Ndunyu, eneo la Kirima.

Polisi wamesema kwamba hakuna yeyote ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo ambalo lilitokea mida ya saa nane unusu usiku wa kuamkia Alhamisi.

Kikosi kinachohusisha maafisa wa polisi na wanajeshi wa KDF wameanza juhudi za kuwawinda washukiwa na kurejesha mifugo ambao waliibiwa.

"Serikali ingependa kuhakikishia wakazi wa Laikipia kuwa juhudi zitawekwa ili kukamata wahalifu hao. Yeyote ambaye analeta vurugu katika eneo hili, siku zake zimehesabiwa" NPS ilitangaza kupitia mtandao wa Twittter.

Takriban wiki mbili zilizopita wiaziri wa usalama wa ndani Fred Matiang'i alitoahakikisho kwa wakazi  wa Laikipia kuwa hali ya utulivu ilikuwa imerejea.

Maafisa zaidi waliongezewa katika maeneo hayo ili kuboresha usalama na kuwafurusha majambazi ambao walikuwa wakihangaisha wakazi.

Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai alihakikishia wananchi kuwa hali ya kawaida ilikuwa imerejea katika maeneo yaliyokuwa yameathirika akidai kuwa majambazi walikuwa wameurushwa tayari.