Hitilafu ya umeme yazua hofu duka la Naivas Ukunda

Muhtasari

• Mteja mmoja Hamisi Ali alisema kwamba aliona cheche za umeme kutoka nyuma.

Image: SHABAN OMAR

Ilikuwa hali ya mguu niponye katika duka la Naivas eneo la Ukunda kufuatia madai ya hitilafu ya umeme.

Ijumaa majira ya asubuhi ilikuwa siku kama ya kawaida yenye shughuli nyingi kwa wanunuzi na wafanyikazi wa duka hilo, nguvu za umeme zilikatizwa kwa ghafla na kama kawaida jenereta ikaanza kunguruma lakini haikufanya kwa muda na ikazima pia.

Ghafla Wafanyakazi, wanunuzi na wale wanunuzi wa kudoea tu dirishani kutoka sehemu ya nyuma ya dukaa walianza kukimbia wakidai kutokea kwa mlio usiokuwa wa kawaida ndani ya duka.

Image: SHABAN OMAR

Kisha king’ora cha kutoa tahadhari ya moto kikaanza kupiga hali ikageuka kuwa mguu niponye.

"Mama yangu, ni nini inafanyika”, baadhi ya walikuwa wakipiga kelele huku wakikimbilia maisha yao.

Walinzi ambao walikuwa mlangoni haraka waliwaongoza wateja waliokuwa wamejawa na hofu hadi katika eneo salama dhidi ya moto.

Mteja mmoja Hamisi Ali alisema kwamba aliona cheche za umeme kutoka nyuma.

"Sijui nimefikaje hapa rafiki yangu, niliacha ndani kila kitu nilichokuwa nikinunua," Ali alisema.

Image: SHABAN OMAR

Muda si muda maafisa wa usalama kutoka kampuni za ARN, SGA walikuwa hapo.

Walifuatwa na kikosi cha kampuni ya umeme nchini KPLC.

Wateja ambao walikuwa wameacha bidhaa zao  ndani walitakiwa kusubiri hadi hitilafu irekebishwe.