Polisi watatu wakamatwa kwa madai ya mauaji

Tukio hilo lilifanyika katika eneo la Kiminini, kaunti ya Trans Nzoia.

Muhtasari

• Maafisa hao wanahudumu katika kituo cha doria cha Big Tree na wanazuiliwa kwenye seli za polisi wakisubiri hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwa mauaji.

• Tukio hilo lilifanyika katika eneo la Kiminini, kaunti ya Trans Nzoia.

 

Pingu
Image: Radio Jambo

Maafisa wawili wa polisi na mmoja wa akiba wamekamatwa kuhusiana na tukio la mauaji.

Watatu hao walitiwa mbaroni siku ya Alhamisi  baada ya mtu anayedaiwa kumpigwa na polisi hao kufariki kutokana na majeraha aliopata wakati akipigwa.

Tukio hilo lilifanyika katika eneo la Kiminini, kaunti ya Trans Nzoia.

Marehemu aliyetajwa kwa jina Robinson Manyonge alifariki Jumatano katika Hospitali ya rufaa ya eneo hilo.

Kulingana na ripoti za polisi na mashahidi marehemu alikuwa abiria kwa pikipiki akielekea nyumbani wakati aliposhambuliwa na maafisa hao wawatu.

Nia ya kumpiga jamaa huyo bado haijabainika.

Maafisa hao wanahudumu katika kituo cha doria cha Big Tree na wanazuiliwa kwenye seli za polisi wakisubiri hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwa mauaji.

Idara ya polisi imekosolewa kwa ongezeko la visa vya polisi kuwashambulia na hata kuwaua wananchi wasiokuwa na hatia.

Makumi ya maafisa wa polisi katika miezi iliyopita wamekamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya washukiwa na watu wengine kwa kiwango cha kutisha.