Pandora Papers Leaks: Uhuru ajibu madai

Uhuru amesema ripoti hiyo itakuwa mwanzo wa ufichuzi wa biashara haramu na ulanguzi wa pesa.

Muhtasari

• Uhuru amesema ripoti hiyo itakuwa mwanzo wa ufichuzi wa biashara haramu na ulanguzi wa fedha. 

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Image: KWA HISANI

Rais Uhuru Kenyatta hatimaye amejibu makala ambayo yamepeperushwa katika vyombo vya habari vya Kimataifa na katika mitandao ya kijamii kuhusu vile familia yake imewekeza kisiri mabilioni ya pesa katika nchi za kigeni.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatatu rais Kenyatta alisema kwamba alivutiwa na makala ya Jumuiya ya Kimataifa ya Uandishi wa Habari za Upelelezi (ICIJ) Pandora Papers leaks na kwamba angependa kutoa taarifa kuhusu makala hayo.

"Umakini wangu umevutiwa na maoni yanayotolewa kuhusu Pandora Papers. Hata ingawa nitajibu kwa undani wakati nitarudi kutoka Ziara yangu ya Kiserikali katika mataifa ya Amerika, wacha niseme hivi...”, taarifa hiyo ilieleza.

"Kwamba ripoti hizi zitasaidia sana kuongeza uwazi na uwadilifu wa kifedha ambao tunahitaji nchini Kenya na kote ulimwenguni. Ulanguzi wa fedha, mapato ya uhalifu na ufisadi unastawi katika mazingira ya usiri na giza. Rais Kenyatta alieleza.

Makala ya Pandora Papers leaks yalidai kwamba familia ya rais Uhuru Kenyatta kwa ushirikiano na viongozi wengine duniani iliwekeza mabilioni ya fedha kisiri katika mataifa ambayo sheria zake zinaruhusu watu ambao wangependa kuficha mali zao kwa sababu moja au nyingine.

Katika taarifa yake Uhuru aliongeza kuwa..."Pandora Papers pamoja na ukaguzi wa baadae utaondoa pazia ya usiri na giza kwa wale ambao hawawezi kuelezea mali zao au utajiri. Asante."

Wakenya sasa watasubiri kwa hamu na ghamu kujua mbivu na mbichi wakati rais Kenyatta atakapotoa taarifa yake kamili kuhusu madai ya Pandora Papers leaks.