Vijana wawili wauawa na wenzao ambao walikataa kurejesha 'memory cards' ambazo walikuwa wameazima

Wawili hao waliuawa na jamaa ambao walikuwa wameazima kadi zao

Muhtasari

•Inadaiwa kuwa wakati Owino alienda kwa Oduori kudai kadi yake, mshukiwa alisita kuirejesha na badala yake akamgonga vibaya hadi akaaga.

•Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya upili ya Brainiac alifariki usiku wa Ijumaa baada ya kudungwa kisu mara mbili kwenye kichwa na kifuani na mwenzake ambaye alisita kumrejeshea 'memory card' yake.

Crime scene
Crime scene

Familia mbili kutoka kaunti ya Nairobi na Busia zinaomboleza vifo vya wapendwa wao ambao walipoteza maisha yao kwenye mizozo miwili tofauti  iliyohusisha kadi ya kuhifadhi data maarufu kama 'memory card'.

Kwenye tukio la kwanza ambalo linaripotiwa kutokea wiki iliyopita katika kaunti ya Busia, jamaa aliyetambulishwa kama Oduori anadaiwa kumuua mwenzake kwa jina Owino ambaye alikuwa amemsaidia na 'memory card' yake kisha kujaribu kuficha yaliyokuwa yametukia.

Kulingana na DCI, Oduori (21) alipendezwa sana na vitu ambavyo vilikuwa vimehifadhiwa kwa 'memory card' ambayo alikuwa amesaidiwa  nayo hadi hakutaka kumrejeshea mwenyewe wakati alienda kuidai.

Inadaiwa kuwa wakati Owino alienda kwa Oduori kudai kadi yake, mshukiwa alisita kuirejesha na badala yake akamgonga vibaya hadi akaaga.

Baada ya kutekeleza unyama huo mshukiwa alimuonya mkewe dhidi ya kuripoti yaliyokuwa yametendeka na kumpa vitisho iwapo angekaidi onyo lake.

Hata hivyo baada ya kubaki kimya kwa kipindi cha wiki moja, mke wa Oduori alishindwa kuficha tena yalikuwa yametukia na akafululiza hadi kituo cha polisi siku ya Ijumaa ambapo alipiga ripoti kuhusiana na mauaji hayo.

Polisi wamemkamata mshukiwa na kuelekzwa katika eneo la tukio ambapo walionyeshwa mahali ambapo inasemekana marehemu alizikwa huku wakisubiri idhini ya kufukua mwili na upasuaji wa mwili.

Kwingineko katika mtaa wa Huruma jijini Nairobi, mwanafunzi mmoja wa shule ya upili anaripotiwa kuuawa kwa kudungwa kisu na rafiki yake ambaye alikuwa ameazima  kadi yake.

Mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu katika shule ya upili ya Brainiac alifariki usiku wa Ijumaa baada ya kudungwa kisu mara mbili kwenye kichwa na kifuani na mwenzake ambaye alisita kumrejeshea 'memory card' yake.

Muuaji alimdunga marehemu kisha akatoweka na kumuacha mhasiriwa wake akilia  kwa uchungu huku dame ikiwa imejaa mwilini. 

Wakazi walijaribu kuokoa maisha ya mwanafunzi huyo kwa kumkimbiza hospitalini ila akaaga alipokuwa anapokea matibabu. Harakati za kumsaka mshukiwa zinaendelea.