Mike Sonko aomba radhi kwa kuchapisha ujumbe wa kupotosha kuhusu kifo cha Charles Njonjo

Muhtasari

•Sonko ambaye alikuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kuchapisha habari za kupotosha kuhusu kifo cha Njonjo amesihi familia ya mwanasiasa huyo wa zamani  pamoja na Wakenya wote wamsamehe akidai kuwa alianguka kwenye mtego wa ripoti zisizothibitishwa.

•Sonko amemtakia Njonjo maisha marefu zaidi duniani licha ya kuwa hapo awali alikuwa amechapisha ujumbe akiombea roho yake ipumzike kwa amani.

Image: HISANI

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameomba radhi kwa kuwa mmoja wa walioeneza uvumi kwamba Charles Njonjo ameaga dunia usiku wa Jumamosi.

Sonko ambaye alikuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kuchapisha habari za kupotosha kuhusu kifo cha Njonjo amesihi familia ya mwanasiasa huyo wa zamani  pamoja na Wakenya wote kwa jumla wamsamehe akidai kuwa alianguka kwenye mtego wa ripoti zisizothibitishwa.

Kupitia kwa ukurasa wake wa Facebook, mwanasiasa huyo amedai kuwa alipotoshwa na ujumbe wa mwanahabari Salim Lone ambaye ni mwandani wa Njonjo.

"Ningependa kuomba msamaha kwa familia ya mwanasheria mkuu wa zamani Charles Njonjo na Wakenya wote kwa kuchapisha habari za kupotosha kuwa Charles ameenda kuwa na Mungu. Hata hivyo, nilijua habari hizo kutoka kwa Bwana Salim Lone ambaye ni rafiki wa karibu wa Charles Njonjo na ambaye pia ameomba radhi kwa kutoa habari hizo za kupotosha" Sonko aliandika.

Sonko amemtakia Njonjo maisha marefu zaidi duniani licha ya kuwa hapo awali alikuwa amechapisha ujumbe akiombea roho yake ipumzike kwa amani.

Salim Lone ambaye aliwahi kuwa msemaji wa kinara wa ODM Raila Odinga pia ameomba radhi kwa kupotosha watu kuwa Njonjo ameaga dunia,

Lone alisema kuwa alikuwa amepatwa na aibu kubwa kufuatia kitendo chake cha kueneza habari ambazo hakuwa amechukua muda kuthibitisha.

"Nahisi vibaya. Nilipakia jumbe hapo awali kuhusu rafiki yangu Charles Njonjo kuwa amefariki. Inaonekana nilikosea kabisa. Haina haja nitaje tovuti nyingi za habari ambazo ziliripoti habari hizo, ningechunguza zaidi. Nahisi aibu kubwa na naomba radhi kwa wale wote ambao walipotoshwa na chapisho langu" Alisema Lone.

Mapema siku ya Jumapili familia ya Njonjo ilipuuzilia mbali uvumi kuhusu kufariki kwake na kudai kuwa ni ripoti zilizotiwa chumvi.

Ujumbe ambao ulitolewa na familia ya mkongwe huyo wa miaka 101 ulithibitisha kuwa Njonjo ako salama salimini na anafurahia wikendi akiwa nyumbani kwake.

Ripoti kuhusu kifo changu zimetiwa chumvi. Niko buheri wa afya na nafurahia wikendi yangu nyumbani tunaposherehekea siku ya Utamaduni" Ujumbe huo ulisoma.

Uvumi kuhusu kifo cha mkongwe huyo wa miaka 101 ulienezwa sana mitandaoni siku ya Jumamosi.