ICJ kutoa uamuzi wa kesi ya mpaka wa bahari ya Hindi kati ya Kenya na Somalia leo

Muhtasari

•Mahakama ya kimataifa ya ICJ ilitangaza kuwa uamuzi wa kesi hiyo utasomawa na  rais wa mahakama jaji Joan E. Donoghue  mida ya saa tisa alasiri.

•Tayari  nchi ya Kenya imeapa kuwa haitatambua uamuzi ambao unatarajiwa kutolewa leo ikilalamika kuwepo kwa upendeleo ulioegemea upande wa Somalia kwenye uendeleshaji wa kesi hiyo.

Eneo linalozozaniwa
Eneo linalozozaniwa
Image: MAKTABA

Hatima ya mzozo kuhusu mpaka wa bahari kati ya Kenya na nchi ya Somalia hatimaye itajulikana leo.

Mahakama ya kimataifa ya ICJ ilitangaza kuwa uamuzi wa kesi hiyo  ambayo ilifikishwa mahakamani na Somalia mwaka wa 2014 utasomwa na  rais wa mahakama jaji Joan E. Donoghue  mida ya saa tisa alasiri.

"Mnamo tarehe 12 Oktoba, mahakama ya kitaifa ya haki pamoja na tawi la haki la muungano wa mataifa (UN) litatoa uamuzi wa kesi inayohusisha ukataji mpaka wa bara hindi kati ya Kenya na Somalia. Kikao cha umma kitafanywa katika Kasri ya Amani, Hague mida ya saa tisa alasiri ambapo rais wa ICJ Jaji Joan E. Donoghue atasoma uamuzi wa korti" Ulisoma ujumbe ambao mahakama ya ICJ ilitoa  kwa wanahabari.

Wahudumu wa mahakama na wawakilishi wa pande zote zilizohusishwa katika kesi ile ndio pekee wataruhusiwa kuwa mahakamani wakati uamuzi huo utakuwa unasomwa. Wengine wote ikiwemo wanahabari na raia watafuata mitandaoni kwa sababu ya mikakati iliyowekwa kudhibiti maambukizi ya COVID 19.

Tayari  nchi ya Kenya imeapa kuwa haitatambua uamuzi ambao unatarajiwa kutolewa leo ikilalamika kuwepo kwa upendeleo ulioegemea upande wa Somalia kwenye uendeleshaji wa kesi hiyo.

Siku ya Ijumaa katibu mkuu katika wizara ya masuala ya kigeni Macharia Kamau alisema kuwa mahakama ya ICJ haina mamlaka ya kuamua mzozo uliopo.

Kenya na Somalia zinazozana kuhusiana na jinsi mpaka wa kutenganisha mataifa hayo mawili katika bahari la Hindi unafaa kuchorwa. Kipande kinachozozaniwa na mataifa hayo mawili kinaaminika kuwa na mafuta.