Nenda nyumbani pamoja na rais Uhuru mwaka wa 2022- Kalonzo amwambia Raila

Kalonzo alisema kuwa kinara wa ODM atakuwa amezeeka na tayari atakuwa amehudumia Wakenya kwa njia nyingi katika kazi yake ya siasa kufikia mwezi Agosti mwaka wa 2022.

Muhtasari

•Kalonzo pia alisisitiza kuwa Raila anakaribishwa kujiunga na OKA iwapo tu lengo lake sio kushurutisha viongozi wengine kumuunga mkono.

•Aliwashukuru rais Kenyatta na Raila kwa kukubali kusalimiana wakati nchi ilikuwa karibu kukabiliwa na ghasia baada ya chaguzi za mwaka wa 2017.

•Kalonzo alisema kwamba ana imani viongozi wengine wa OKA watamchagua kupeperusha bendera.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka
Image: MERCY MUMO

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amesisitiza kuwa rais Kenyatta anafaa kustaafu pamoja na mwenzake Raila Odinga muhula wake utakapokamika mwaka ujao.

Kalonzo alisema kuwa kinara wa ODM atakuwa amezeeka na tayari atakuwa amehudumia Wakenya kwa njia nyingi katika kazi yake ya siasa  kufikia mwezi Agosti mwaka wa 2022.

Alipokuwa kwenye mahojiano katika stesheni moja nchini asubuhi ya Jumatani, makamu huyo wa rais wa zamani hata hivyo aliwashukuru rais Kenyatta na Raila kwa kukubali kusalimiana wakati nchi ilikuwa karibu kukabiliwa na ghasia baada ya chaguzi za mwaka wa 2017.

"Nafikiria rais Uhuru anafaa kuenda nyumbani na Raila. Ukiangazia umri wa wagombeaji wengine wote wa kiti cha urais Raila ametuacha sana" Kalaonzo alisema.

Kalonzo pia alieleza matumaini yake kwamba wenzako wa One Kenya Alliance (OKA) ; Gideon Moi (Kanu), Moses Wetangula (Ford Kenya) na Musalia Mudavadi (ANC) watamuunga mkono kupeperusha bendera ya muungano huo.

Viongozi wote wanne wa OKA wametangaza kuwa watagombea kiti cha urais.

Kalonzo pia alisisitiza kuwa Raila anakaribishwa kujiunga na OKA iwapo tu lengo lake sio kushurutisha viongozi wengine kumuunga mkono.

Pia alisihi jamii ya Kalenjin kutoongozwa na hisia wakati watakuwa  wanachagua viongozi wao mwaka ujao.

"Msiongozwe na hisia mwaka wa 2022. Mnafaa kutupilia mbali msemo 'lazima iwe mtu wetu'" Kalonzo alisema.

Alisema kuwa jamii ya Kalenjin ina historia kubwa na ile ya Kamba na uhusiano kati ya jamii hizo mbili unafaa kuongezwa nguvu.

"Tuko na historia kubwa pamoja. Sijakuja hapa kuhubiri ukabila lakini lazima tujikumbushe kuhusu uhusiano wetu" Alisema.

Kiongozi huyo wa Wiper alitangaza kuwa amepanga msururu wa ziara katika eneo la bonde la  ufa ili kujipigia debe kwa jamii ya Kalenjin.

"Nitakuja kanisani kuabudu nanyi. Nitafanya mikutano katika sehemu mbalimbali za bonde la ufa" Alisisitiza.

Aliomba jamii ya Kalenjin kumkaribisha akidai kuwa naibu rais William Ruto huwa anakaribishwa vizuri anapozuru eneo la Ukambani.

Kalonzo alisema kwamba ana imani viongozi wengine wa OKA watamchagua kupeperusha bendera.

(Utafsiri: Samuel Maina)