Hofu baada ya mwili wa polisi anayeaminika kujitoa uhai kupatikana ndani ya basi Nairobi

Muhtasari

•Mwili wa Konstabo Martin Thairu (40)  ulipatikana na jeraha la risasi kichwani siku ya Jumatano mida ya jioni.

•Inaaminika kuwa Thairu alijipiga risasi kupitia kwenye mdomo wake usiku wa Jumanne akiwa ndani ya basi lililokuwa limezuiliwa kituoni kama ushahidi.

Kitanzi
Kitanzi
Image: HISANI

Polisi wanachunguza kisa ambapo mwili wa afisa mmoja ambaye anatuhumiwa kujitoa uhai ulipatikana ndani ya basi lililokuwa limeegeshwa ndani ya kituo cha polisi cha Diplomatic jijini Nairobi.

Mwili wa Konstabo Martin Thairu (40)  ulipatikana na jeraha la risasi kichwani siku ya Jumatano mida ya jioni. Bunduki yake aina ya AK47 ambayo inaaminika kutumika kutekeleza kitendo hicho ilipatikana kando ya mwili wake

Inaaminika kuwa Thairu alijipiga risasi kupitia kwenye mdomo wake usiku wa Jumanne akiwa ndani ya basi lililokuwa limezuiliwa kituoni kama ushahidi.

Polisi walisema kuwa walishinda wakimtafuta marehemu tangu asubuhi ya Jumatano baada yake kukosa kufika kazini. 

Alipokuwa anathibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi katika eneo la Nairobi Augustine Nthumbi alisema kuwa bado haijabainika wazi kilichosababisha tukio hilo.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya afisa mwingine aliyekuwa anafanya kazi katika kituo cha DCI cha Parklands kupatikana akiwa amejitoa uhai ndani ya nyumba yake maeneo ya Kasarani.