Mume ni ‘mshukiwa’ baada ya mwanariadha wa Kenya Tirop kupatikana amefariki

Polisi walipoingia nyumbani, walimkuta Tirop kwenye kitanda na kulikuwa na damu sakafuni,

Muhtasari

•Mshikilizi wa rekodi ya ulimwengu mkenya Agnes Tirop alipatikana ameuawa kwa kuchomwa kisu nyumbani kwake katika mji wa Iten magharibi mwa Kenya

•Uchunguzi wa jinai sasa unaendelea juu ya kifo chake, na polisi wanasema mumewe ametoweka.

Image: GETTY IMAGES

Mshikilizi wa rekodi ya ulimwengu mkenya Agnes Tirop alipatikana ameuawa kwa kuchomwa kisu nyumbani kwake katika mji wa Iten magharibi mwa Kenya, polisi wakimchukulia mumewe kama mshukiwa .

Mshindi huyo mara mbili wa medali ya shaba ya Mashindano ya Riadha ya Dunia, ambaye alimaliza wa nne katika fainali ya Olimpiki ya mbio za mita 5,000 miezi miwili iliyopita, alikuwa na umri wa miaka 25.

Uchunguzi wa jinai sasa unaendelea juu ya kifo chake, na polisi wanasema mumewe ametoweka.

Siku ya Jumatano, wachunguzi wa eneo la uhalifu walikuwa nyumbani kwa Tirop, ambaye polisi wanasema aliripotiwa kupotea na baba yake Jumanne usiku.

"[Polisi] walipoingia nyumbani, walimkuta Tirop kwenye kitanda na kulikuwa na damu sakafuni," Tom Makori, mkuu wa polisi wa eneo hilo, alisema.

"Waliona alikuwa amechomwa kisu shingoni, jambo lililotupelekea kuamini ni jeraha la kisu, na tunaamini kwamba ndicho kilichosababisha kifo chake.

"Mumewe bado hajulikani aliko , na uchunguzi wa awali unatuambia kuwa mumewe ni mshukiwa kwa sababu hawezi kupatikana. Polisi wanajaribu kumtafuta mumewe ili aweze kuelezea kilichomsibu Tirop."

Makori ameongeza kuwa polisi wanaamini kuwa CCTV katika nyumba hiyo inaweza kusaidia uchunguzi wao.

Tirop pia alikutwa na jeraha la kuchomwa tumboni mwake, vyanzo vimeiambia BBC