Wakongwe wanne waliotuhumiwa kuwa wachawi wateketezwa Kisii

Walishukiwa kuteka nyara na kuroga mwanafunzi wa shule ya upili

Muhtasari

•Watatu kati ya walioteketezwa walikuwa wanawake ilhali mmoja alikuwa mwanaume mwenye umri wa takriban miaka 80.

•Wanawake wawili kati ya washukiwa hao wanne walisshutumu wenzao wawili na walikuwa wa kwanza kuteketezwa papo hapo.

•Polisi kutoka Kisii walitambulisha marehemu kama Jemima Mironga 60, Agnes Ototo 57, Sigara Onkware 62 na Sindege Mayaka 85. 

Vifaa vya kufanyia uchawi
Vifaa vya kufanyia uchawi
Image: MAKTABA

Wanakijiji wanne wakongwe waliteketezwa wakiwa hai siku ya Jumapili baada ya kutuhumiwa kuwa wachawi.

Wanne hao waliuawa katika kijiji cha Nyagonyi, eneo la Marani Kisii kufuatia tukio  la utekaji nyara wa mwanafunzi wa shule ya sekondari ambaye alipatikana barabarani akiwa amepoteza fahamu.

Inasemekana kwamba mwanafunzi huyo ambaye hapo awali alionekana mdhaifu alikuwa ametekwa nyara usiku katika hali tatanishi.

Wanakijiji walipomtemea mate alirejesha fahamu, akaanza kuzungumza na kuibua kizaazaa kikubwa pale.

Watatu kati ya walioteketezwa walikuwa wanawake ilhali mmoja alikuwa mwanaume mwenye umri wa takriban miaka 80.

Polisi walisema kuwa eneo la tukio tayari lilikuwa limeteketezwa wakati walipowasili.

Wakazi walisema kuwa wanne ambao waliteketezwa walikuwa miongoni mwa genge la wachawi ambao walidanganya mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyagonyi wakati alikuwa anasoma usiku wa Jumamosi.

Wanakijiji walisema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa amerogwa na kudhulumiwa hapo awali.

"Nadhani hii ni mara ya nne kama sio ya tano ambapo wanamteka nyara" Mkazi aliyejitambulisha kama John Getuma alisema.

"Amekuwa mdhaifu kila wakati. Hata wazazi wake wameuza kila kitu ili kugharamia matibabu yake" Getuma alisema.

Wanawake wawili kati ya washukiwa hao wanne walisshutumu wenzao wawili na walikuwa wa kwanza kuteketezwa papo hapo.

Mwanamke mmoja alivutwa kutokana nyumbani kwake ambako alikuwa amejifungia. Nyumba yake pia iliteketezwa.

"Mwanzoni hatukujua kilichokuwa kimefanyika lakini wakati nilienda karibu tulipata mvulana akiwa amelala chini. Kila mtu aliagizwa  amtemee mate. Tulipomtemea mate, alianza kuzungumza na hapo ndipo wanawake wale walichukuliwa na kuteketezwa" Mkazi aiyejitambulisha kama Moraa aliambia wanahabari.

Mwanamke mwingine na mwanaume mmoja waliteketezwa baada ya kutajwa na washukiwa wa kwanza.

Polisi kutoka Kisii walitambulisha marehemu kama Jemima Mironga 60, Agnes Ototo 57, Sigara Onkware 62 na Sindege Mayaka 85. 

Vijana ambao walikuwa wamejihami waliendeleza msako  wakitazamia kutambua wachawi wengine katika kijiji hicho.

(Utafsiri: Samuel Maina)