Mbunge wa Kitutu Chache alaani vikali mauaji ya wakongwe wanne waliohusishwa na uchawi Kisii

Mauaji ya wakongwe hao yalihusishwa na mgogoro wa shamba

Muhtasari

•Angweyi amewasihi wakazi wa  eneo bunge analowakilisha kusita kuchukua sheria mikononi na badala yake kuwapeleka watuhumiwa wa uchawi kwa polisi.

•Angweyi aliwahimiza maafisa wa polisi kufanya upesi katika kukamata waliotekeleza mauaji yale wikendi iliyopita.

Vifaa vya kufanyia uchawi
Vifaa vya kufanyia uchawi
Image: MAKTABA

Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angweyi amelaani vikali mauaji ya wakongwe wanne waliotuhumiwa kufanya uchawi katika eneo la Marani Kisii siku ya Jumapili.

Angweyi amewasihi wakazi wa  eneo bunge analowakilisha kusita kuchukua sheria mikononi na badala yake kuwapeleka watuhumiwa wa uchawi kwa polisi.

Alipokuwa anahutubia wanahabari nje ya bunge la kitaifa siku ya Jumanne, Angweyi aliwahimiza maafisa wa polisi kufanya upesi katika kukamata waliotekeleza mauaji yale wikendi iliyopita.

Haya yanajiri wakati  tayari polisi wakiwa  wamekamata washukiwa wawili wakuu wa mauaji ya wakongwe hao wanne.

Mauaji ya wakongwe hao ambayo yamekemewa vikali mitandaoni yalihusishwa na mgogoro wa shamba.

Amos Nyakundi Ondiek na kijana mwingine mwenye umri wa miaka 18 wanazuiliwa katika kituo cha polisi huku uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo ukiendelea.

Wawili hao walikamatwa siku ya Jumatatu baada ya msako mkubwa  dhidi ya waliohusika kwenye mauaji yale kuanzishwa. Vikosi vya maafisa vilitumwa katika eneo la Marani ili kuwawinda wote amabo walihusika.

Washukiwa zaidi wanatarajiwa kutiwa mbaroni wakati uchunguzi na msako zaidi unapoendelea.