Uchunguzi wa maiti wabaini kilichosababisha kifo cha mwanariadha Agnes Tirop

Marehemu atazikwa nyumbani kwa wazazi wake katika kaunti ya Nandi siku ya Jumamosi.

Muhtasari

•Wanapatholojia walioendeleza shughuli hiyo ya masaa matatu walisema kwamba sababu kuu iliyopelekea  kifo cha Tirop ilikuwa majeraha ya kisu.

•Daktari Dorothy Njeru ambaye aliongoza shughuli hiyo alisema kwamba walikuwa wametayarisha ripoti na kukabidhi maafisa wa DCI ili  waendeleze uchunguzi.

Agnes Tirop
Image: Hisani

Upasuaji wa maiti umebaini kwamba mwanariadha Agnes Tirop alifariki kutokana na majeraha yaliyosababishwa na kisu shingoni na kugongwa na kugongwa na kifaa butu kichwani.

Upasuaji wa mwili wa Tirop  ulifanyiwa na wanapatholojia wawili katika hospitali ya Iten siku ya Jumanne. Wanafamilia pamoja na maafisa wa DCI walikuwepo.

Wanapatholojia walioendeleza shughuli hiyo ya masaa matatu walisema kwamba sababu kuu iliyopelekea  kifo cha Tirop ilikuwa majeraha ya kisu.

Daktari Dorothy Njeru ambaye aliongoza shughuli hiyo alisema kwamba walikuwa wametayarisha ripoti na kukabidhi maafisa wa DCI ili  waendeleze uchunguzi.

Baada ya shughuli hiyo kukamilika mwili ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti huku matayarisho ya mazishi yakiendelea.

Marehemu atazikwa nyumbani kwa wazazi wake katika kaunti ya Nandi siku ya Jumamosi.

Wanafamilia pamoja na maafisa wa shirika la riadha nchini walithibitisha kwamba matayarisho ya mazishi yalikuwa yanaendelea vizuri.

Mwili wa Tirop ulipatikana na majeraha ya kisu mnamo Oktoba 13.

Mpenzi wake Ibrahim Rotich alikamatwa kufuatia hayo na kufikishwa katika mahakama ya Iten siku ya Jumatatu.

Hakimu Charles Kutwa aliamuru Rotich azuiliwe kwa siku 20 zaidi ili kupatia nafasi uchunguzi kukamilika.

Mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Eldoret anaposubiri kesi dhidi yake itajwe tena mnamo Novemba 9.