Mahakama yatoa nafasi kuapishwa kwa gavana mpya wa Nairobi

Muhtasari

• Korti ya Rufaa iliongeza kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya maagizo yaliyotolewa na Mahakama Kuu na maagizo yaliyotafutwa katika ombi la Sonko katika mahakama ya rufaa.

Anne Kananu akiapishwa naibu gavana wa Nairobi, Januari 15, 2021.
Anne Kananu akiapishwa naibu gavana wa Nairobi, Januari 15, 2021.
Image: EZEKIEL AMINGA

Mahakama ya Rufaa imekataa kutoa maagizo yoyote ya kuzuia kuapishwa kwa Ann Kananu kama Gavana wa kaunti ya Nairobi na kusitisha rufaa iliyowasilishwa na Mike Sonko.

Sonko aliwasilisha rufaa katika mahakama ya Rufaa baada ya mahakama kuu kutoa uamuzi kuwa mchakato uliopelekea kutimuliwa kwake kama gavana ulifuata sheria.

Akisikitishwa na uamuzi huo, Sonko alikwenda katika mahakama ya Rufaa akitafuta maagizo ya kumzuia Kananu kuapishwa kama gavana wa Kaunti ya Nairobi.

Majaji wa Korti ya Rufaa Wanjiru Karanja, Jamila Mohamed na Jessie Lessit walitupilia mbali ombi lake kwa sababu kwamba suala la kuapishwa kwa Kananu halikutolewa katika kesi ya Mahakama Kuu na uamuzi uliotolewa na korti hiyo hiyo haukushughulikia au kuamua suala hilo.

"Suala la kuapishwa kwa Kananu halikuwa msingi wa Rufaa katika rasimu ya Sonko. Katika rasimu hiyo ya rufaa, Sonko anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu ambayo ilikataa kutengua mchakato wa mashtaka," walisema.

Korti ya Rufaa iliongeza kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya maagizo yaliyotolewa na Mahakama Kuu na maagizo yaliyotafutwa katika ombi la Sonko katika mahakama ya rufaa.