Seneta Anuar kushtakiwa baada ya kujisalimisha kufuatia madai kuwa alipiga mwanadada risasi

Anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nanyuki akisubiri kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.

Muhtasari

•Polisi walisema kwamba huenda akashtakiwa kwa makosa ya utumizi mbaya wa bunduki, kusababisha majeraha kwenye mwili wa mhasiriwa kati ya makosa mengine.

•Bi Makena alikimbizwa katika hospitali ya Nanyuki akiwa na jeraha ya risasi kwenye mguu wake wa kulia.

•Polisi walisema kwamba bado hawajabaini kilichosababisha tukio hilo la risasi ila wanapanga kuhoji mashahidi zaidi

Image: HISANI

Seneta wa Lamu, Anuar Loitiptip alijisalimisha kwa polisi siku ya Jumapili kufuatia madai kwamba alipiga mwanadada risasi maeneo ya Nanyuki.

Seneta huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nanyuki akisubiri kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.

Polisi walisema kwamba huenda akashtakiwa kwa makosa ya utumizi mbaya wa bunduki, kusababisha majeraha kwenye mwili wa mhasiriwa kati ya makosa mengine.

Bunduki yake ilichukuliwa wakati alijisalimisha alasiri ya Jumapili na itachambuliwa kama sehemu ya uchunguzi.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso alithibitisha kujisalimisha na kukamatwa kwa mwanasiasa huyo.

"Seneta wa Lamu amejisalimisha kufuatia tukio la hapo awali ambapo rafikiye mwanamke alipigwa risasi na kujeruhiwa. Kwa sasa anasaidia polisi na uchunguzi." Bw. Shioso alisema.

Anwar anasemekana kuambia polisi kwamba alishambuliwa akiwa kwa eneo la burudani, jambo ambalo llilifanya afyatue risasi na kujeruhi Joy Makena (32).

Bi Makena alikimbizwa katika hospitali ya Nanyuki akiwa na jeraha ya risasi kwenye mguu wake wa kulia. Aliambia polisi kwamba alipigwa risasi na seneta Anwar.

Mhasiriwa alisema kwamba mabishano yalianza kati yake na seneta huyo wa muhula wa kwanza kabla yake kuchukua bunduki na kumpiga risasi kwa karibu.

Mwanasiasa huyo anaripotiwa kukimbia na kuacha mlinzi wake na wafuasi wengine wampatie huduma ya kwanza. Anuar anadaiwa kupigia mwanasiasa mmoja mashuhuri simu akiomba kusaidiwa kuwasiliana na mkubwa wa DCI.

Mashahidi walisema kwamba tukio hilo lilitokea mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia Jumapili wakati kikundi kidogo cha watu kilikuwa kimekutana kwa uwanja wazi.

Baadae polisi walipata mlinzi wa Anuar na kuchukua bastola yake ambayo ilikuwa na risasi 13. Vibweta viwili ya risasi ambavyo vilikuwa vimetumika vilipatikana katika eneo la tukio.

Polisi walitembelea mhasiriwa hospitalini na kumhoji kuhusiana na tukio hilo.

Maafisa wale walisema kwamba bado hawajabaini kilichosababisha tukio hilo la risasi ila wanapanga kuhoji mashahidi zaidi.

Sio mara ya kwanza kwa Anuar kupatikana kwa drama kwani mwaka wa 2019 alijeruhiwa pamoja na biti ya Sonko kwenye mashambulio ya watu wasiojulikana maeneo ya Kasarani, Nairobi.

(Utafsiri: Samuel Maina)